DAR-ES-SALAAM: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikamilike.
Akizungumza na kamati za usalama za mikoa na wilaya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mikoa kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mtandao akiwa katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni, Dar es Salaam.
“Kwenye eneo la usimamizi wa miradi, wakuu wa mikoa hakikisheni mnazo taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo; hii ni fursa yenu ya kujua benki tuliyonayo ya utekelezaji wa miradi yote ya tangu mwaka 2021,” alisema.
Aliongeza, “angalieni ni miradi gani imepata fedha na mjiridhishe kama imekamilika au la na kama bado haijakamilika, fuatilieni ni kwa nini haijakamilika.”
SOMA: Samia awa mbogo rushwa miradi ya maendeleo
Majaliwa amesema miradi inayojengwa kwa fedha za serikali kwenye halmashauri na manispaa ni mingi amesisitiza ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba mwaka huu ili ianze kutumika mapema.
“Matumizi ya miradi hii ndiyo faraja kwa wananchi na ndiyo matamanio yao,” alisema.
Pia Majaliwa alihimiza viongozi wafuatilie uzalishaji wa chakula kuhakikisha Tanzania inakuwa na ziada ya kutosha. “Tanzania tumezalisha chakula kingi na tuna ziada, wakuu wa mikoa na wilaya jukumu lenu kusimamia kilimo na uzalishaji uwe umefikia malengo na wenye ziada.
“Pia fanyeni sensa ya kujua mazao ya kwenye maghala, uhifadhi wake ni mzuri na je, kinatosha? Tuwe na takwimu za kutosha juu ya chakula tulicho nacho kwenye hifadhi yetu,” alisema.
SOMA: https://www.pmo.go.tz/
Wakati huohuo, Majaliwa alisisitiza makusanyo yote ya fedha kwenye halmashauri na manispaa ni lazima yaingizwe benki ndipo yapangiwe matumizi.
“Hata kama si fedha za msaada kutoka kwenye taasisi au asasi zisizo za kiserikali, ni lazima DC (Mkuu wa Wilaya) ajue ili atoe taarifa kwa RC (Mkuu wa Mkoa). Ma-RC wasimamie mtiririko wa fedha kwenye halmashauri,” alisema.
Aliongeza: “Suala la usimamizi wa mapato ya serikali liwe ajenda ya kudumu. Tusipofanya hivyo, tutashindwa kutekeleza mipango yetu. Mmemsikia rais wetu Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuhusu ukusanyaji wa mapato, ambayo baadaye yanaletwa kwenye maeneo yenu ili kutekeleza miradi”.
Maeneo mengine aliyoyawekea msisitizo kwenye kikao hicho ni pamoja na utatuzi wa kero za wananchi, udhibiti na uhifadhi wa mazingira, nishati safi ya kupikia, ulinzi na usalama, kilimo cha umwagiliaji, magonjwa yasiyoambukiza, maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 na ushirikiano baina ya viongozi wa serikali na wa CCM. Kikaokazi hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa.