Samia awa mbogo rushwa miradi ya maendeleo
RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya wakwamishaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ya umeme kwa kuendekeza rushwa, undugu na urasimu usiokuwa na sababu za msingi akisema kufanya hivyo ni kuliangamiza taifa.
Sambamba na hilo amesema serikali haitawafumbia macho watendaji ‘wanaopiga dili’ katika miradi ya maendeleo kwa sababu wanasababisha wakandarasi wasiokuwa na sifa kupata kazi au kupitisha miradi iliyo chini ya viwango vinavyotakiwa.
Rais Samia alisema hayo jana wakati wa utiaji saini mikataba 26 ya mradi wa uimarishaji wa gridi ya taifa (Gridi Imara) na umeme vijijini wenye thamani ya Sh trilioni 1.9 kwa mwaka utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne kwa jumla ya Sh trilioni 4.42.
Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya wakandarasi wa kampuni mbalimbali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likiwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Maharage Chande na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) chini ya Mkurugenzi Mkuu, Hassan Said Ikulu, Dar es Salaam.
Alisema zipo mamlaka ambazo zina jukumu la kupitisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuombewa fedha ili ujenzi uanze lakini mamlaka hizo zimejigeuza na kuwa wakwamishaji wakubwa wa miradi ya maendeleo kwa sababu zisizo na msingi.
“Natambua kuna wenzetu wengi ambao walikuwa na mkandarasi wake mkononi na alipenda apate, kwa sababu hakupata fitina ni nyingi mbio PPRA, mbio Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), mbio sijui wapi nenda ule mradi usifanyike uzuiwe…kwa matakwa yake binafsi, hatutakwenda,” alisema.
Aliongeza kuwa ili miradi hiyo ya umeme na mingine ya maendeleo ifanyike haraka inahitaji maamuzi ya haraka na kwamba mtu anapokosa alichokitaka na kuamua kwenda Takukuru au PPRA kuizuia anakwamisha miradi hiyo kuanza.
Rais Samia aliwataka watendaji katika taasisi hizo zinazoletewa pingamizi kupima wanacholetewa kabla ya kufanya maamuzi, akiongeza kuwa mtu mmoja akikosa maslahi katika zabuni hizo bila kuangalia maslahi ya nchi anaweza kukwamisha maendeleo ya nchi.
“Ule muda ambao mradi unachukua mwaka mzima bila kupata maamuzi hapana, tukiamua pesa ipo mradi uende ukafanywe kama mtu hakupata ina maana hakufikia vigezo kama angefikia vigezo angepata,” aliongeza.
Alitoa onyo kwa wakaguzi wa miradi wanaoendekeza rushwa kutoka kwa wakandarasi na kupitisha miradi mibovu kuwa hawastahili kuwepo katika nafasi zao kwa sababu wameshindwa kuheshimu taaluma zao.
Rais Samia alisema suala la vibali vya ajira nalo linatakiwa kutazamwa kwa sababu kuna mashirika yanataka vibali vya haraka vya ajira lakini yanaletewa mlolongo mrefu wa taratibu ili kuweza kupata vibali vya kuajiri na wanazungushwa mwaka mzima.
Alisema katika utendaji watu wote wanaorudisha nyuma maendeleo waondolewe haraka na kama watu hao wapo katika mamlaka yake waletwe kwake ili achukue hatua za haraka miradi iende mbele.
Aliwataka watendaji kufanya kazi kwa bidii na kuonesha wanaweza ili wasiondolewe katika nafasi zao na kuwataka wote wanaoondolewa wasijisumbue kwenda ofisini kwake kupeleka malalamiko kwa sababu kama kweli wanasababisha kukwama kwa miradi ni lazima waondoke.
Alisema mabadiliko katika mashirika yapo kwa watendaji wazembe na wababaishaji ila njia rahisi ya kuyakwepa ni kufanya kazi na sio kukaa tu kusubiri mgao katika fedha za miradi zisiwapite.
Rais Samia aliwataka wawekezaji wa nje kufuata makubaliano kulingana na makubaliano ya pamoja wakati wa kusaini mikataba ya miradi ya maendeleo akiongeza kuwa serikali haitakubali nyongeza ya masharti kwa sababu kama jambo katika nchi halikubaliki kwa vyovyote vile halitakubaliwa.
“Tuzungumze hadi tuelewane, kinyume na hapo nenda kwa sababu mradi ni wetu unatekelezwa nchini kwetu na wewe unakuja na masharti yako unayaweka katika mradi wetu. Hapana lazima tuzungumze tukubaliane, kama hapana basi wawekezaji wapo wengi, wengi tu,” alisema.