Tanzania ina viwanda 1,604 mafuta ya kula

DODOMA; Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Tanzania ina jumla ya viwanda 1,604 vya kuzalisha mafuta ya kula, huku kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 14 na kwamba serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta hayo.
Kapinga ametoa taarifa hiyo leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kati ya viwanda hivyo, 1,038 ni vidogo sana, 543 ni vidogo, tisa ni vya kati na 14 ni vikubwa na kueleza kuwa viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa wa kuzalisha tani 2,527,739 za mafuta ya kula kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Kapinga, viwanda hivyo vimetoa ajira za moja kwa moja 10,755 na zisizo za moja kwa moja 36,416 na kuwa uzalishaji wa mafuta ya kula nchini bado haujakidhi mahitaji ya soko la ndani.
“Kwa sasa viwanda vinazalisha tani 302,000 za mafuta ya kula wakati mahitaji ya nchi ni takriban tani 700,000 kwa mwaka. Hivyo, tani 430,000 huagizwa kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya ndani,” amesema Kapinga.
Ameeleza kuwa serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ikiwemo kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa wakulima, kutoa ruzuku ya mbolea, kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu za mafuta pamoja na kuboresha teknolojia kwa wasindikaji wadogo.
Katika hatua nyingine, Kapinga amesema katika mwaka 2025/2026, kiwanda cha Vion Win Ltd cha kukamua na kusafisha mafuta ya alizeti pamoja na kuzalisha mashudu ya chakula cha mifugo kimejengwa mkoani Singida kwa gharama ya mtaji wa shilingi bilioni 5.5.
Amesema hadi kufikia Aprili 2026, kiwanda hicho kimezalisha ajira za moja kwa moja 70 na zisizo za moja kwa moja 300, huku kikiwa na uwezo wa kuchakata tani 100 za mbegu za alizeti kwa siku.
Vilevile, Waziri Kapinga amesema kiwanda cha Mainland Group Agro Process Co. Ltd kilichopo Dodoma kimefanya upanuzi wa uzalishaji kutoka tani 75,000 hadi tani 150,000 za mbegu za alizeti kwa mwaka.



