Posta Tanzania waja kisasa zaidi

KIGOMA; SHIRIKA la Posta Tanzania limesema limeanza kufanya maboresho makubwa katika utoaji huduma ya kusafirisha vifurushi nje ya nchi, ikiwemo kutumia mtandao wa kompyuta kumuwezesha mteja kufuatilia mzigo wake tangu ulipokabidhiwa kwa shirika hilo hadi ulipo kwa wakati huo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta, Ferdinand Kabyemela amesema mpango huo unalenga kuondoa dhana iliyojenga kwa Watanzania wengi kwamba mizigo inayosafirishwa na shirika hilo inachukua muda mrefu kufika na wakati mwingine kupotea.
Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, shirika limeanza mkakati wa kuhakikisha vifurushi vinavyotumwa vinachukua siku chache tangu vilipokabidhiwa kwao, hadi kufika vinapotakiwa kwenda na kwamba hiyo itajenga imani na kuwafanya wateja kurudisha uzalendo katika kutumia huduma za shirika hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Posta wa Shirika hilo, Arube Ngaruka amesema kupitia Huduma za Haraka Usafirishaji Vifurushi (EMS), wameingia mkataba na mashirika sita ya ndege kusafirisha mizigo, hali ambayo itawezesha mizigo kufika haraka na kwa usalama.
Pia amesema kwa sasa mzigo unaweza kuchukuliwa nyumbani au eneo la biashara la mteja na kusafirishwa kwa haraka na kwa bei nafuu.

Naye Meneja wa Shirika la Posta Kigoma, Ndagije Chobaliko alisema kuwa mazao ya uvuvi ya Ziwa Tanganyika, ikiwemo dagaa na samaki yamepata soko kubwa nchi za Marekani na Canada, hivyo wameanza kampeni kwa wasafirishaji wa mazao hayo kuona namna ya kutumia huduma za shirika hilo.



