Imani ya wawekezaji yawezesha hatifungani EFTA kuvuka lengo

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) imesema kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika masoko ya mitaji nchini, sambamba na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali, kumechangia mafanikio ya hatifungani ya kampuni ya Equity for Tanzania (EFTA) kuvuka kiwango kilicholengwa.
Akizungumza leo wakati wa kuorodheshwa rasmi kwa hatifungani hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Bw Nicodemus Mkama, alisema mafanikio hayo yanaonesha jinsi wawekezaji wanavyoendelea kuamini EFTA pamoja na mfumo mzima wa masoko ya mitaji nchini.
Hatifungani hiyo ilifanikiwa kukusanya takribani shilingi bilioni 33.4, zaidi ya mara mbili ya lengo la awali la shilingi bilioni 15, hatua iliyotajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa ya mauzo ya hatifungani katika miaka ya karibuni.
Bw Mkama alisema mwitikio mkubwa wa wawekezaji ni ushahidi kuwa sera za serikali zinazolenga kukuza ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za kiuchumi na kuimarisha sekta ya fedha zinaendelea kuzaa matunda.
Alieleza kuwa maboresho mbalimbali yaliyofanywa na serikali pamoja na wadhibiti wa sekta hiyo yamewezesha kuwepo kwa mazingira rafiki yanayochochea ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.
Miongoni mwa hatua zilizochangia mafanikio hayo ni kupunguzwa kwa kiwango cha chini cha uwekezaji kutoka shilingi milioni moja hadi laki tano, jambo lililoruhusu wananchi wengi zaidi, hususan vijana na wanawake, kushiriki katika fursa za uwekezaji ambazo hapo awali zilionekana kufikiwa zaidi na wawekezaji wakubwa.
“Mafanikio ya hatifungani hii siyo tu ishara ya imani kwa EFTA, bali pia yanaonesha kuwa wawekezaji wana imani kubwa na masoko ya mitaji pamoja na mfumo wa udhibiti uliowekwa na serikali,” alisema Bw Mkama.
Aidha, alisema matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na kampeni za elimu ya fedha zilizotolewa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa sekta ya fedha zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika masoko ya mitaji.
Alisema fedha hizo zitatumika kusaidia upatikanaji wa matrekta, mashine za kilimo, vifaa vya uchakataji, mitambo ya ujenzi, vifaa vya migodi pamoja na magari ya mizigo na utalii.
Aliongeza kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa vifaa hivyo kutachochea uzalishaji kwa biashara ndogo na za kati, hasa zile zinazopata changamoto kupata mikopo ya kawaida kutoka benki.
Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Bw Nicomed Bohay, alisema mwitikio mkubwa wa wawekezaji unaakisi imani waliyonayo katika mfumo wa biashara wa taasisi hiyo pamoja na mikakati yake ya muda mrefu.
Alisema EFTA imekuwa ikipanua vyanzo vya fedha kwa kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya fedha za muda mrefu zinazopatikana kupitia masoko ya mitaji ya ndani.
“Matokeo haya yanaonesha kuwa masoko ya mitaji nchini yana uwezo mkubwa wa kufadhili sekta za uzalishaji na kusaidia ukuaji wa uchumi,” alisema Bw Bohay.
Aliongeza kuwa EFTA inalenga kusaidia kundi la wafanyabiashara wanaoitwa “missing middle”, yaani wale wenye mahitaji makubwa ya kifedha ambayo hayawezi kuhudumiwa kikamilifu na taasisi ndogo za fedha lakini pia hawafikiwi kwa urahisi na mfumo wa kawaida wa benki.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya EFTA, Profesa Andrew Temu, alisema mafanikio ya hatifungani hiyo yanatoa ishara chanya kuhusu uimara na uaminifu wa mfumo wa usimamizi wa sekta ya fedha nchini.
Alisema hatua hiyo itahamasisha taasisi nyingi zaidi, za umma na binafsi, kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Profesa Temu alisema EFTA itaendelea kusimamia vizuri rasilimali zake ili kuhakikisha uwekezaji unachangia kupunguza umaskini, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.



