Majaliwa aagiza somo la michezo kufundishwa shuleni

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Elimu, TAMISEMI na Wizara ya Utamaduni kuhakikisha somo la michezo linafundishwa shuleni kwa kuwa waalimu wa somo hilo wapo katika chuo cha Malya na Butimba.

Akizungumza leo Aprili 13, 2023 bungeni jijini Dodoma alipokutana na mabingwa wa soka Afrika kwa shule za sekondari, timu ya Fountain Gate waliofika bungeni hapo, Majaliwa pia ameagiza mchezo wa Netiboli upewe kipaumbele na uanze kufanyika.

Majaliwa ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuratibu vyema mashindano mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi ambayo yameendelea kuitangaza vyema Tanzania pamoja na uongozi wa Fountain Gate.
“Naupongeza uongozi wa shule hii pamoja na Alliance ya jijini Mwanza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuunga mkono maendeleo ya Sekta ya Michezo nchini, tunawashukuru sana naamini mtaendelea kufanya hivyo katika michezo mingine”. Amepongeza Majaliwa.

Awali akizungumza Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dk Pindi Chana amesema wizara itaendelea kuratibu mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa kuwa ni miongoni mwa mashindano yanayozalisha wachezaji wengi.

Habari Zifananazo

Back to top button