Majaliwa ataka kasi ujenzi barabara ya mzunguko

Majaliwa ataka kasi ujenzi barabara ya mzunguko

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma waongeze kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango.

Majaliwa alitoa agizo hilo Jumapili alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara hiyo ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma.

“Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda. Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati,” alisema.

Advertisement

Majaliwa pia aliagiza wahandisi wasimamizi wa mradi huo wasimamie wakandarasi ili barabara hiyo ijengwe kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi.

Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Majaliwa aliwataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vinabaki salama.

“Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango,” alisema.

Majaliwa aliiagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waweke utaratibu wa kuwaweka pamoja vijana wanaoshiriki kwenye ujenzi wa miradi nchini ili waweze kutumika zaidi kwenye kampuni za ujenzi za wazawa.

Kaimu Meneja Tanroads Mkoa wa Dodoma, Salome Kabunda alisema mradi huo utasaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma na umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, utekelezaji wa mradi huu utawezesha kujengwa kwa vituo vya afya vinne katika mitaa ya Mahomanyika, Veyula, Nala na Ihumwa. Pia yatanunuliwa magari ya wagonjwa manne katika vituo hivyo,” alisema Kabunda.

Alisema sehemu ya kwanza ya ujenzi huo ni babaraba kutoka Nala-Veyula-Mtumba hadi bandari kavu ya Ihumwa (Km 52.5) inayotakiwa kuchukua muda wa miezi 39 kukamilika.

“Sehemu ya pili ya ujenzi wa barabara hii ni kutoka Bandari kavu ya Ihumwa-Matumbulu hadi Nala (Km 60) ulioanza Septemba 01, 2020 utagharimu shilingi bilioni 120.8 kwa muda wa miezi 43,” alisema Kabunda.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

 

 

 

/* */