Majaliwa atoa maagizo kukuza biashara

DAR-ES-SALAAM: SERIKALI imeagiza wizara zinazohusika na viwanda, biashara na uwekezaji zihakikishe zinabuni mbinu za kukuza na kusaidia biashara ndogo na za kati.
Akizungumza na wadau wa sekta binafsi jijini Dar-es-salaami kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 inaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
“Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo na ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za kati kukua na kuchangia katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya kuimarisha sekta binafsi,” alisema Majaliwa.
Pia ameziagiza wizara na taasisi za serikali ziendelee kupokea maoni ya sekta binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika marekebisho ya sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na kuboresha taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara kwa kuwezesha upatikanaji wa vibali na leseni kwa haraka na kwa urahisi.
Majaliwa amesema maendeleo yaliyopo nchini hivi sasa yametokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali na sekta binafsi.
“Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu katika kila sekta yanategemea mchango wa serikali pamoja na sekta binafsi.
SOMA: https://tpsftz.org/
Dhamira na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta binafsi ili ihuishwe na kuwa mshindani katika kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu,” alisema.
Majaliwa amesema serikali imeimarisha mazingira ya biashara kwa kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Hatua hizi zimejumuisha kuboresha taratibu za usajili wa biashara, kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, kutoa fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, nishati, miundombinu, utalii, viwanda na kuanzisha maeneo maalumu ya uwekezaji,” alisema.
SOMA: Rais Samia bega kwa bega sekta binafsi
Majaliwa alisema serikali imewekeza katika miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji na mawasiliano ambayo ni muhimu kwa shughuli za uwekezaji na biashara ili kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuasisi falsafa mpya ya kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo kuondoa ukiritimba wa mawazo.
“Rais wetu yeye anaamini na anakiri katika dhana ya kusikiliza sauti na mawazo ya wengine ili kuweka mazingira bora ya mahusiano kati ya sekta binafsi na serikali,” alisema Jenista.
Amesema kupitia falsafa hiyo Rais Samia amefanya vikao vya kubadilishana mawazo mara kwa mara na makundi tofauti ya sekta binafsi ili kusikiliza changamoto, kujifunza mafanikio na kutengeneza mfumo wa kusongambele kwa manufaa ya pande zote mbili.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema mwaka huu wa fedha wizara hiyo imeweka vipaumbele sita ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Naye Mwenyekiti wa TPSF, Angelia Ngalula alisema wanatamani kuona Tanzania inakuwa kitovu cha biashara Afrika kutokana na rasilimali ilizonazo.
“Pia tunatamani kuona biashara nyingi zinarasimishwa na wigo wa walipakodi unaongezwa,” alisema Ngalula.



