Elimu ya msingi sasa kidigitali

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imechukua hatua kubwa ya kuimarisha elimu ya msingi kwa kuboresha mitaala na kuwajengea uwezo wa kutumia mifumo ya kidijiti kupitia ushirikiano na Kampuni Sahara Consult.
Hatua hiyo ilifikiwa jana Dar es salaam pande hizo mbili ziliposaini mkataba wa makubaliano (MoU)wa kufanya kazi pamoja wakilenga kuimarisha matumizi ya teknolojia ya elimu katika shule za msingi.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo,Leo jijini dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Anneth Komba, alisema ajenda kubwa ya ushirikiano huo ni kuimarisha matumizi ya teknolojia katika mfumo wa elimu ya msingi.
Amesema ushirikiano wao utaweka msingi wa kuimarisha elimu ya kidijitali nchini kupitia kuboresha mitaala, kuwajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia pamoja na kuwaunganisha wabunifu wa teknolojia na watunga mitaala.
Ameeleza kuwa TET inaamini umefika wakati muafaka wa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili kuhakikisha kunakuwa na wahitimu wenye stadi za karne ya 21.
“Ajenda yetu kubwa ni kuimarisha teknolojia ya elimu katika mfumo wa elimu ya msingi. Serikali ya Awamu ya Sita ilileta mageuzi makubwa na katika maboresho hayo yameleta mabadiliko mbalimbali katika mitaala yetu na sehemu ya mabadiliko ni matumizi ya TEHAMA,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Komba, makubaliano hayo yanajumuisha majukumu 12, yakiwemo kuongoza mapitio ya mitaala kwa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine yanajumuishwa katika ufundishaji na ujifunzaji, ikiwemo uandaaji wa programu kuanzia Darasa la Tatu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Consult, Jumanne Mtambalike amesema makubaliano hayo yanalenga kufanya kazi kwa pamoja kutumia ubunifu, teknolojia na ujasiriamali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Alisema watafanya kazi kwa karibu na shule za serikali na binafsi zinazoshirikiana na TET ili kuona namna teknolojia na ubunifu vitakavyosaidia kuboresha elimu.
Mtambalike amesema pia watafanya kazi kwa karibu na wabunifu wa teknolojia za elimu, kuwaunganisha na Taasisi ya Elimu Tanzania pamoja na watunga mitaala ili bunifu zao ziendane na mahitaji ya mitaala iliyoboreshwa.



