Miti 1,000 yapandwa Tanga

TANGA: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Tanga, imekuja na mkakati wa kuhifadhi mazingira kwa kuzindua kampeni ya upandaji wa miti 1,000 katika shule mbalimbali za msingi na sekondari jijini hapa.
Zoezi hilo, lililolenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, limezinduliwa rasmi katika Shule ya Sekondari Ummy Mwalimu, iliyopo Kata ya Maweni, Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Kamishna wa Huduma za Ufundi wa TRA, Ted Silkiliwasha, alisisitiza kuwa upandaji wa miti ni hatua muhimu ya kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazotokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.
”Miti inazalisha hewa ya Oxygen kwa wingi. Ukiwa na miti mingi, Taifa linaweza kunufaika kupitia masoko ya hewa ukaa (Carbon Credits), jambo linaloongeza pato la Taifa. Tunatamani miaka 30 ijayo tutakapokuja kutathmini matokeo ya miti tunayoipanda leo, tuone mabadiliko chanya ya kimaendeleo,” alisema Silkiliwasha.
Naibu Kamishna huyo alitumia fursa hiyo kuhamasisha utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari kama nguzo ya ujenzi wa uchumi imara.
Aliiagiza shule hiyo kuanzisha ‘Klabu ya Elimu ya Mlipakodi’ ili kuwajengea wanafunzi uzalendo wa kodi tangu wakiwa wadogo.
“Niwaombe wanafunzi, nendeni mkawe mabalozi wa elimu ya kodi katika familia zenu na jamii inayowazunguka. Tujenge utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari ili kuijenga nchi yetu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, alibainisha kuwa zoezi hilo ni sehemu ya shughuli mbalimbali za kijamii zinazofanywa na mamlaka hiyo katika mkoa wa Tanga kuadhimisha kilele cha miaka 30.
“Tunapoadhimisha miaka hii 30, tumejipanga kutoa huduma bora zaidi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla. Tunawakaribisha wafanyabiashara wenye changamoto yoyote kujitokeza ofisini kwetu ili kuzitatua, hasa wakati huu tunapoelekea kukamilisha mwaka wa fedha,” alisema Castro.



