Majaliwa: Serikali iko imara huduma za jamii

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali iko imara na itaendelea kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii zinawafikia wananchi kwa ukaribu.

Alisema hayo jana alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kuimarisha utoaji wa huduma na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

“Kituo cha afya cha Rais Samia kinakuwa na huduma zote muhimu zikiwemo za upasuaji, wodi ya wanawake na watoto, wodi za akinababa na akinamama, magonjwa mchanganyiko, hii ndio dhamira yetu,” alisema.

Majaliwa alisema ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya unaoendelea nchini unahusisha hospitali za rufaa za kanda, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati.

Akizungumzia kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Majaliwa alisema kuwa serikali imesambaza wakandarasi wa umeme nchi nzima vikiwemo vijiji vya Wilaya ya Ruangwa ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote.

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwataka viongozi wa mikoa wahakikishe wanabainisha wafugaji katika vijiji vyao ili kuwatambua pamoja na mifugo yao ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji. Alitoa wito kwa wafugaji nchini kuweka utaratibu wa kufuga mifugo ambayo wanaweza kuihudumia.

“Hakuna mwenye haki zaidi ya mwenzake. Ukiamua kufuga fuga mifugo ambayo unaweza kuihudumia, usilishe kwenye mashamba ya watu, kufanya hivyo mkono wa sheria utakufuata,” alisema.

Alizitaka pia serikali za vijiji kuhakikisha zinasimamia sheria ya kutolima ndani ya mita 60 kutoka kwenye mito na vyanzo vingine vya maji ili kuhifadhi vyanzo hivyo.

Akizungumza na wananchi wakati alipokagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mbwemkuru, Majaliwa alikipongeza kikundi cha vijana cha Ukaje Ujenzi kwa kuamua kuanzisha umoja huo na kufanya kandarasi mbalimbali za serikali.

Mwenyekiti wa kikundi hicho akizunguamza kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekuwa fursa kwao ya kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.

Habari Zifananazo

Back to top button