Majaliwa: Serikali imedhamiria kuwawezesha wachimbaji wadogo

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wainuke kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa pato la taifa pamoja na kukuza vipato vyao binafsi.

Amesema hayo leo Juni 24 jijini Dodoma wakati akizindua rasmi mitambo 10 ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo yenye thamani ya shilingi bilioni 12.41 iliyonunuliwa na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sambamba na vitendea kazi vya Shirika hilo kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Shirika.

Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa madini, wachimbaji pamoja na wananchi.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ndiyo maana Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 imeelekeza kuwasaidia kwa kuwatengea maeneo, kuwawezesha kufanya utafiti, kuwapatia mitambo ya uchorongaji na uchimbaji wa madini kwa njia za kisasa,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha kuwa mitambo hiyo ni mwendelezo wa juhudi zilizowekwa na Serikali ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mitambo mitano Oktoba 2023 ambayo tayari imeanza kutumika na kutoa mchango mkubwa kwa wachimbaji.

Kupitia mitambo hiyo, wachimbaji wadogo wameanza kuaminiwa na taasisi za kifedha, hivyo kuongeza uwezo wao wa kukopesheka.

Aidha, amesema mitambo miwili kati ya hiyo 10 imetengwa mahususi kwa ajili ya kuwahudumia wanawake wachimbaji, ikiwa ni sehemu ya kujumuisha jinsia zote katika fursa za kiuchumi kupitia sekta ya madini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button