Makadirio bajeti ya serikali 2026/27 Sh Tril 61

DODOMA; BAJETI ya Seikali kwa mwaka 2026/27, nakadiriwa kuwa Sh Tril 61, Bunge limeelezwa.
–
Hayo yamesemwa bungeni leo Februari 2, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Mussa Omar akiwasilisha , mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati (2026/27 – 2028/29).
“Katika kipindi cha muda wa kati (2026/27 – 2028/29), Serikali inatarajia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 204,087.7, sawa na wastani wa shilingi bilioni 68,029.2 kwa mwaka.
“Aidha, kwa mwaka 2026/27, bajeti ya Serikali inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 61,934.2,” amesema Waziri Omar na kuongeza kuwa:
“Katika kipindi cha muda wa kati, mapato ikijumuisha misaada yanakadiriwa kuwa wastani wa shilingi bilioni 52,480.8, sawa na ukuaji wa wastani wa asilimia 12.1.
“Kwa mwaka 2026/27, mapato yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 46,691.3, ambapo mapato ya kodi ni shilingi bilioni 36,889.3, mapato mengine ni shilingi bilioni 9,238.8 (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya shilingi bilioni 1,966.2) na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi bilioni 563.1.
“Ongezeko hilo limezingatia misingi ya uchumi jumla na mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato ikiwemo kuhimiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika malipo na ukusanyaji wa mapato.
“Kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi, urasimishaji wa sekta isiyo rasmi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji yatakayowezesha uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato,” amesema.
Awali leo kabla Waziri Omar hajawawasilisha bungeni mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo, aliwasilisha nyenzo tatu zitakazowezesha kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Muda mrefu wa miaka 25 (2026/27 hadi 2050/51), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka mitano (2026/27 hadi 2030/31) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27.



