Makalla ataja siri ushindi uchaguzi mitaa

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeainisha sababu zilizokipo ushindi wa kishindo na kusababisha anguko kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, mwaka huu.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alieleza hayo leo Novemba 29,2024 katika mkutano uliofanyika na waandishi wa habari Dar es salaam akitoa shukrani kwa wananchi kwa ushindi waliouoata katika uchaguzi huo.

“jana tumeshuhudia Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mchengerwa ametangaza matokeo ya uchaguzi na nyie ni mashahidi kwambamatokeo yaliyotangazwa yameipa ushindi CCM wa kishindo katika mitaa asilimia 98.8 vitongoji asilimia 98 wajumbe wa vijiji asilimia 99 na wajumbe wa mtaa asilimia 99,”amesema Makalla

Advertisement

Aidha Makalla amesema sababu ya kwanza ya ushindi wao ni kuridhika kwa wananchi na kazi kubwa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 ya CCM katika kutekeleza miradi ambayo ipo katika kata, mitaa, biji na vitongoji ambayo inaonekana na wananchi, hivyo imesaidia wananchi kujenga imani kwa CCM.

Pia amesema sababu nyingine ni kuwa na maandalizi ya kutosha katika kujiandaa na uchaguzi huo kwani walikuwa wanajua wanakabiliana na uchaguzi mwaka huu hivyo walitumia muda mwingi kufanya maandalizi.

“Kwanza Chama Cha Mapinduzi kilifanya tathmini ya viongozi waliopo katika mitaa, vijiji na vitongoji kwahiyo kila wilaya ilifanya tathmini ya viongozi waliopo madarakani na changamoto za wananchi kwahiyo CCM haikukosea kuteua wagombea safi wanaokubalika,”amesema Makalla.

Ameongeza kuwa CCM kuanzia ngazi ya shina mpaka taifa walijitoa na kushiriki kwa kiasi kikubwa na ushiriki huo umepelekea wao kuibuka na ushindi na kugusia kuwa maandalizi kwa vyama vya upinzani yalikuwa mdogo na kupelekea anguko lao.

Makalla amesema anaamini walikuwa na maandalizi mazuri kwani hatarajii kusikia watu wakisema CCM wameshindaje kwa sababu walijiandaa kwa kuanza na kufanya ziara katika mikoa 20.