Makalla: CCM itashinda kwa kishindo

KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi, Siasa na Mafunzo, Amos Makalla amesema chama hicho kimejipanga kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kibamba na Kawe Dar es Salaam jana, alisisitiza kuwa CCM haina mashaka katika kushika dola na kwamba uchaguzi huo ni muhimu kwa chama hicho.

Alisema chama hicho kimezindua kampeni rasmi Novemba 20, 2024 na tayari kimejiandaa kushinda kwa kishindo katika maeneo yote nchini.

Advertisement

“Katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, tutashinda kwa kishindo. Kampeni zetu zinaendelea vizuri na tunatarajia ushindi mkubwa,” alisema.

Alisema chama chake kimeweka wagombea kwa asilimia 100 katika mitaa, vijiji na vitongoji vyote nchini na hakuna nafasi iliyosalia bila wagombea.

Alisema vyama vingine baadhi havikusimamisha wagombea, jambo ambalo linadhihirisha kutokuwa na utayari wa kushindana.

“Vyama vingine havina utayari, mpaka sasa kuna mitaa ambayo hakuna washindani. Wapinzani wanaofikiri wanaweza kuiangusha CCM kwa kura za hapana wanajidanganya, kwani wanashindwa hata kusimamisha wagombea,” alisisitiza Makalla.

Alisema CCM itaendelea na kampeni zake huku wapinzani wakijiunga. Alisema chama kinaimarisha umoja ili kupata ushindi wa kishindo.

Aidha, alisema wamefanya vikao na kumaliza tofauti za wagombea walioonesha nia ya kugombea lakini hawakuteuliwa katika kura za maoni. Alisema, “Hakuna mtu anayekatwa katika uchaguzi bali hawakuteuliwa tu.”