DAR ES SALAAM; Makampuni 130 kati ya 700 yamepata tuzo ya kuzitambua kutokana na ufanisi na kuzalisha bidhaa bora barani Afrika.
Tuzo hizi za makampuni bora barani Afrika (ACOYA) zimeandaliwa
na The Global CEOs Institute wakishirikiana na Eastern Star Consulting Group Tanzania zimekuwa chachu ya kuongeza ufanisi na uzalishaji wa bidhaa bora na zenye viwango ili kuleta tija katika ukuaji wa maendeleo na uchumi ndani ya Afrika.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Eastern Star Group of Tanzania Deogratius John Kilawe wakati wa hafla ya kuwatunukia tuzo makampuni 130 yaliyofanya vizuri barani Afrika kwa mwaka 2024 iliyofanyika jijini Dar es salaam.
“Lengo ni kutambua mchango mkubwa wa makampuni yanayofanya vizuri barani Afrika na kuwapongeza na kuwapa moyo ili waendelee kufanya vizuri zaidi ili kuhudumia soko la Afrika kwa huduma na bidhaa zenye ubora wa hali ya juu zitakazoweza kupambana na soko la dunia pamoja na kukuza uchumi wa nchi za Afrika Kwa ujumla’ Alisema.
Kilawe amesema kuwa pamoja na mambo mengine ikiwa ni msimu wa pili wa tuzo hizo zilizoanza mwaka 2023 na kuleta mafanikio ya kuwaleta kwa pamoja makampuni makubwa zaidi Afrika na kujadili mambo mbalimbali yatakayosaidia katika kukuza uchumi wa Afrika pamoja na kuwatunukia tuzo makampuni yaliyofanya vizuri zaidi.
Pia aliongeza kuwa Kwa mwaka huu ni zaidi ya nchi 20 makampuni 700 yameshiriki katika tuzo hizo ambapo zimepatikana kampuni bora 130 na kuwapatia tuzo ili kuchochea ufanisi na katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Tuzo hizo pia zimehudhuriwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Shabani Omary pamoja na viongozi mbalimbali ambapo kampuni za Petrol Group Tanzania, Mansoor industries na Sunking green planet wameibuka vinara wa Tuzo hizo.