Makandarasi ‘goigoi’ waikera serikali

SERIKALI imeiagiza Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuwachukulia hatua za kisheria makandarasi wanaokiuka wajibu wao ikiwamo kutekeleza miradi ya serikali chini ya kiwango na thamani ya fedha iliyokusudiwa.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya ametoa agizo hilo jana jijini Mbeya katika mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi uliolenga kujadili namna ya kujenga uwezo wa makandarasi wa ndani, mafanikio na changamoto zao.

Kasekenya alisema dhamira ya serikali ni kuona miradi mikubwa ya ujenzi nchini inatekelezwa na makandarasi wa ndani, lakini wameshindwa kufikia hatua hiyo.

Aliitaja sababu ya kushindwa ni kutokana na makandarasi hao kukosa uzalendo wa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati na ubora na thamani ya fedha iliyokusudiwa.

“Changamoto kubwa kwa makandarasi wa ndani ni kukosa wataalamu wa kusimamia miradi, uhaba wa wataalamu wa ubobezi ujenzi wa miradi mikubwa, pamoja na kutokamilisha kazi kwa muda na kwa ubora ulikusudiwa,” alisema Naibu Waziri.

Alisema ukosefu wa vifaa vya ujenzi wa miradi ikiwamo changamoto ya kukosekana kwa mitambo mikubwa ya ujenzi wa miundombinu kama barabara, imesababisha makandarasi wengi wa ndani kutekeleza miradi wanayopewa chini ya kiwango kilichokusudiwa.

Msajili wa CRB, Rhoben Nkori alisema bodi hiyo inatekeleza hatua mbalimbali katika kujenga imani kwa makandarasi wa ndani ikiwamo ukaguzi wa miradi wanayotekeleza sambamba na kuwafutia usajili makandarasi wote wanaobainika kutojihusisha kikamilifu na shughuli za ukandarasi kwa muda mrefu.

“Kwa mwaka 2022 bodi ilisajili makandarasi 1,341 na kufanya idadi ya waliosajiliwa kufikia 14,034, idadi ya usajili imeongezeka kwa wastani wa 900 kwa mwaka hata hivyo makandarasi 520 waliobainika kukiuka taratibu hizo walifutiwa usajili,” alisema Nkori.

Makandarasi walioshiriki mkutano huo wameiomba serikali iweke sera mahususi itakayowahusisha wadau wote katika jukumu la kuwajengea uwezo makandarasi wa ndani kwa maslahi ya uchumi wa nchi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button