Makardinali kuanza kukutana Mei 7 kumchagua Papa

DAR ES SALAAM; MAKARDINALI 135 watakutana Mei 7, mwaka huu katika kongamano la kumchagua kiongozi wa Kanisa Katoliki.
Taarifa kutoka Vatican zinaeleza mkutano huo wa faragha utaanza ndani ya Kanisa la Sistine Mei 7, mwaka huu.
Makardinali watakutana kwenye mchakato huo kumpata mrithi wa Papa Francis aliyeaga dunia Aprili 21, mwaka huu katika makazi yake Casa Santa Marta na alizikwa Aprili 26.
Kwa upande wake, Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni alisema makardinali watashiriki Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na wanaostahili kupiga kura watakusanyika katika Kanisa la Sistine kwa kura ya siri.
Baada ya kuingia kwenye kanisa la Sistine makardinali hao hawataruhusiwa kuwa na mawasiliano na yeyote wa nje hadi papa mpya atakapochaguliwa.
Kuna duru moja tu ya upigaji kura mchana wa kwanza wa kongamano hilo lakini watapiga kura hadi mara nne kila siku baadaye.
Papa mpya anahitaji kura ya theluthi mbili na hilo linaweza kuchukua muda.
Kila Kardinali anapiga kura kwenye kadi rahisi inayosema kwa Kilatini: “Ninamchagua kama Papa Mkuu” na anaongeza jina la mgombea wao aliyechaguliwa.
Iwapo mkutano huo utamaliza siku ya tatu bila kufikia uamuzi, makardinali wanaweza kutulia kwa siku ya sala.
Nje ya kanisa la Sistine wafuatiliaji na waumini duniani watakuwa wakitazama ishara ya moshi mweupe kutoka kwenye bomba la moshi.
Ikiwa moshi ni mweusi kutakuwa na duru nyingine ya kupiga kura. Moshi mweupe unaashiria kuwa papa mpya amechaguliwa