Makumbusho Isimila mshindi mawasilisho ya urithi

MAKUMBUSHO ya Zama za Mawe Isimila yaliyopo mkoani Iringa yametangazwa kuwa mshindi miongoni mwa mawasilisho bora ya urithi na utafi ti wa pamoja kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Makumbusho (ICOM 2025) unaomalizika leo Roma, Italia.
Hayo yalisemwa na Mhifadhi Mambo ya Kale Mkuu kutoka Kituo cha Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Magomeni, Neema Mbwana ambaye anashiriki katika mkutano huo akiambatana na Benedict Jagadi Mhifadhi Msaidizi na Amina Salum, Mhifadhi Mwandamizi.
“Ushindi huu umepatikana baada ya andiko nililoandika kuhusu makumbusho haya lililowasilishwa kwenye mashindano ya kitaaluma yajulikanayo kama ICOM na likachaguliwa miongoni mwa washindi,” alisema Neema.
Alisema ushindi huo unaonesha thamani ya kipekee ya Makumbusho ya Isimila kama eneo lenye zana za mawe za zaidi ya miaka 300,000, nguzo za asili na historia inayounganisha mabara.
Neema alisema wasilisho lilijikita katika kuonesha muunganiko na mfanano wa Isimila na Hifadhi ya Taifa Ruaha ambapo pia imejaaliwa kuwa na nguzo za asili.
Vilevile, Tanzania kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imeshiriki, ikiwasilisha maono ya kulinda urithi huo
kupitia ushirikiano, uhifadhi endelevu na ushirikishwaji wa jamii.