Malaiguanani kuhamasisha upigaji kura Oktoba

ARUSHA: VIONGOZI wa Milla wa Jamii ya Kifugaji ya Kimasai maarufu kwa jina la ‘Malaiguanani’ Wilaya ya Longido mkoani Arusha wameahidi kumtafutia kura za kishindo mgombea urais wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuhamashisha wananchi wa jimbo hilo kupiga kura.
Mwenyekiti wa Malaiguanani Longido, Simon Melau amesema hayo leo Septemba 29, 2025 mara baada ya kikao cha Malaiguanani kutoka katika tarafa nne za jimbo hilo ambazo ni pamoja na Tarafa ya Longido, Ketumbeine ,Engaranaibor na Enduemit.
Amesema kuwa shukrani pekee kwa wananchi wa jimbo hilo ambao wengi wao ni wafugaji ni kumpa kura za kishindo Samia kwa kuwa miradi imetekelezwa kwa asilimia mia moja kwa kusimamiwa na mbunge wa jimbo hilo Dk Steven Kiruswa.
Melau amesema wananchi wa Jimbo la Longido walikuwa na changamoto kubwa ya majisafi na salama ya kunywa na kwa ajili ya mifugo lakini chini ya uongozi wa Rais Samia ameweza kufanikiwa kupeleka mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 60 kutoka chanzo ya maji cha Mto Simba Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro hadi Mjini Longido umbali wa zaidi ya km 50 kitu ambacho hakikutekelezwa toka kuanzishwa kwa wilaya hiyo .
Amesema upatikanaji wa maji kwa sasa ni asilimia 80 na wananchi wa Longido wananufaika na mradi wa maji na kutoa adha kwa akina mama na watoto kwenda umbali mrefu kusaka maji nyakati za usiku na alfajiri na kuhatarisha maisha yao kwa wanyama wakali.
Mwenyekiti huyo amesema pamoja na kumpa kura za kishindo Rais pia watahakikisha mgombea ubunge wa jimbo la Longido,Dk Kiruswa naye anapata kura za kutosha kwani naye ameweza kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo ikiwemo maji, afya, elimu na barabara hivyo anastahili kurudi katika wadhifa huo bila ya wasiwasi wowote.
Naye, Laiguanani Thomas Ole Ngulupa amesema kura za Rais katika Jimbo la Longido zitakuwa za kumwagika kwa kuwa jamii ya kifugaji wakiwemo vijana,wanawake na wazee wamemkubali mgombea huyo wa Urais wa CCM kwa kufanya mambo makubwa katika Wilaya ya Longido hivyo hawana sababu ya kuacha kumpa kura.
Ngulupa amesema kila mwenye macho ameona Jimbo la Longido sio Jimbo lile la miaka ile hivyo fadhila mkubwa kwa wana Longido ni kumpa kura nyingi na za kutosha Samia sambamba na mgombea ubunge wake Kiruswa.
Laiguanani mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kelembu Ole Kitoo alisema viongozi wa milla kwa umoja wao katika vikao vyao vya Milla vilivyokaa wameazimia kumpa kura za kishindo Rais akiwemo Mbunge na madiwani wote wa CCM waliopita biloa kupingwa.
Kitoo amesema uamuzi wa kumpa kura Rais huo ni wa viongopzi wote wa Milla katika Jimbo la Longido ambao watakuwa wakipita kila nyumba kueleza sifa za Samia ikiwa ni pamoja na kuifanya Longido kuwa bora kimaendeleo kuliko wilaya yoyote ya Kifugaji mkoani Arusha.