WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa ameagiza maofisa utumishi wa taasisi za halmashauri zote nchini wasimamie kuhakikisha malipo ya malimbikizo ya watumishi wote yanalipwa kwa wakati.
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza katika hafla ya siku ya mwalimu duniani wilayani Bukombe na kusema kuwa ni lazima stahiki za watumishi ikiwemo walimu zilipwe kwa wakati.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Dk Samia Suluhu imejidhatiti kupunguza kama siyo kumaliza madai ya watumishi ikiwemo walimu ili kuhamasisha utendaji na uwajibikaji wao mahala pa kazi.
Amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 kuelekea 2024/25 serikali malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 144,326 yenye gharama ya Sh bilioni 229.9 na malipo yanaendelea.
“Maofisa utumishi muende mkaangalie eneo hili, pale ambapo watumishi wanahitaji kulipwa stahiki zao, iwe ni malimbikizo tunahitaji orodha yao ili serikali ilipe hatuhitaji mgogoro na watumishi.
“Kwa sasa lugha ya malimbikizo sasa tumeanza kuifuta kidogo kidogo ambapo kila mtu anapopandishwa daraja anapandishwa mshahara mpya papo hapo na kwa wakati.
“Malipo mbalimbali ya stahiki ya walimu kwenda kusoma na likizo, mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, wote ni lazima walipwe,” alisema Majaliwa.
Amesema ndani ya kipindi hicho pia serikali imeruhusu takribani watumishi 36,768 kubadilishiwa kada ambapo takribani sh bilioni tatu zimetumika kulipa kutoka muundo wao wa sasa.
“Suala la upandishaji wa madaraja pia limekaa vizuri chini ya ofisi ya Rais wizara ya utumishi, ambapo watumishi 601,698 wamepandishwa madaraja ikiwemo walimu,” amesema Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu ameagiza walimu kuendelea kuwekewa mazingira bora ya kazi, uratibu wa mafunzo kazini, kushirikiana na CWT, tathimini ya mara kwa mara ya elimu na ushiriki katika michezo mbalimbali.
Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Bukombe, Dk Dotto Biteko amesema walimu ndio nguzo ya taaluma zingine na hivo serikali imejidhatiti kuendelea kushirikiana nao kwa wakati wote.
Dk Biteko amesema ni wajibu wa walimu wanapoadhimisha siku ya mwalimu duniani kuendelea kuzingatia utendaji wenye tija huku akiwataka viongozi wengine kuwapa nafasi walimu kwa maendeleo ya elimu.