Benki ya ushirika yaimarisha mkakati uchumi jumuishi

DAR ES SALAAM: BENKI ya Ushirika (Coop Bank) imeendelea kuimarisha mkakati wake wa kukuza uchumi jumuishi kwa kuongeza kiwango cha utoaji mikopo kwa sekta ya kilimo, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea uzalishaji nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah, amesema benki imejipanga kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia upanuzi wa huduma za kifedha kwa makundi ambayo kwa muda mrefu hayajafikiwa kwa urahisi.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa benki hiyo, mafanikio yaliyopatikana yanatokana na utekelezaji thabiti wa mkakati wa muda wa kati uliosaidia kuimarisha huduma na kuongeza imani ya wateja.
Kwa mujibu wa takwimu za robo ya kwanza ya mwaka 2026, kitabu cha mikopo kimeongezeka kwa kasi na kufikia sh bilioni 101.02 kutoka bilioni 16.6 mwaka uliopita, sawa na ukuaji wa asilimia 506. Ukuaji huo unaashiria kupanuka kwa utoaji mikopo katika sekta mbalimbali za uchumi.
Vilevile amesema viashiria vingine vya kifedha vinaonesha mwelekeo chanya, ambapo jumla ya mali za benki zimefikia shilingi bilioni 178.7 kutoka bilioni 46.8 mwaka 2025, huku amana za wateja zikiongezeka hadi sh bilioni 101.5 kutoka bilioni 12.5, ikiwa ni ongezeko la asilimia 709.
Katika upande wa wateja, benki imerekodi ongezeko kubwa kutoka wateja 5,000 hadi zaidi ya 37,000, hali inayoonesha kuimarika kwa uaminifu na matumizi ya huduma zake.
Katika juhudi za kuendeleza ujumuishaji wa kifedha, benki imeanzisha huduma za kidijitali zikiwemo Coopesa, Coop Net na Coop Wakala, zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi, hasa katika maeneo yasiyofikiwa kirahisi na matawi ya benki.
Ng’urah ameongeza kuwa benki hiyo inalenga kufikia familia milioni 10 ambazo hazina huduma rasmi za kifedha, huku ikiendelea na mpango wa kufungua matawi mapya katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Kagera, pamoja na kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa gharama nafuu.



