Mameneja Posta kuwekwa kwenye mizani ya matokeo

DAR ES SALAAM: Shirika la Posta Tanzania limeelekeza mwelekeo mpya wa usimamizi wa utendaji kwa kuweka matokeo ya biashara, ufanisi wa matumizi ya rasilimali na ubora wa huduma kuwa vigezo muhimu vya kupima uwajibikaji wa viongozi wake.
Chini ya msisitizo huo, mameneja wa mikoa pamoja na viongozi wa makao makuu watapimwa kwa mafanikio wanayoyapata katika kukuza biashara na kuboresha huduma, huku wale watakaoshindwa kutimiza majukumu yao wakikabiliwa na hatua za uwajibikaji baada ya tathmini ya utendaji.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema hakuna kiongozi atakayekuwa nje ya wigo wa tathmini hizo, akisisitiza kuwa nafasi ya uongozi itaambatana na wajibu wa kuonesha matokeo yanayopimika.
Mbodo ameyasema hayo Novemba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa mameneja wa mikoa kuhusu usimamizi wa utendaji unaozingatia matokeo na kuongeza uzalishaji.
Amesema tathmini hizo zitafanyika kwa kuzingatia mazingira na matokeo ya kila eneo, huku watendaji wanaoonesha mafanikio wakitambuliwa na maeneo yenye changamoto yakifanyiwa uchambuzi ili kubaini hatua za kuboresha utendaji.
Akitoa mfano wa fursa za kibiashara zinazoweza kuchochea ukuaji wa shirika hilo, Mbodo ametaja Mkoa wa Morogoro ambao umepata fursa kubwa katika biashara ya usafirishaji wa vifurushi, hali iliyosababisha mahitaji ya huduma kuongezeka na kuibua changamoto ya upungufu wa magari.

Amesema meneja wa mkoa huo amejiwekea lengo la kusafirisha vifurushi 5,000, akisisitiza umuhimu wa menejimenti kuhakikisha inatoa rasilimali na ushirikiano unaohitajika ili kutekeleza lengo hilo.
Kwa mujibu wa Mbodo, mafanikio ya aina hiyo yanapaswa kutumika kama msingi wa kujifunza kwa mikoa mingine, kukuza ubunifu wa kibiashara na kupanua matumizi ya fursa zilizopo katika soko la huduma za posta.
Katika hatua nyingine, amesema Tanzania imefikia nafasi ya 66 duniani na ya nne barani Afrika katika tathmini ya Umoja wa Posta Duniani (UPU), ikiwa nyuma ya Misri, Morocco na Mauritius.
Hata hivyo, amesema shirika hilo linakusudia kuimarisha nafasi yake katika ushindani wa kimataifa na kujenga uwezo wa kuwa kinara wa huduma za posta barani Afrika.
Ameeleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani ameonesha matarajio ya Tanzania kufikia nafasi hiyo kutokana na mageuzi yanayoendelea katika sekta ya posta nchini.
Akihitimisha, Mbodo amewataka mameneja kutumia mafunzo hayo kuimarisha usimamizi wa biashara, matumizi ya rasilimali na uwajibikaji wa watumishi, akisisitiza kuwa mageuzi ya shirika yanahitaji ushiriki wa kila mtumishi.
Amesema Posta Tanzania ni mali ya wananchi, hivyo mafanikio yake yanapaswa kupimwa kwa uwezo wa kutoa huduma bora, kujiendesha kwa ufanisi na kuongeza mchango wake katika uchumi



