Mamia wamuaga Sarungi, azikwa

KIONGOZI mstaafu wa serikali, Profesa Philemon Sarungi ameagwa na kuzikwa Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Profesa Sarungi alikuwa mtu mwenye misimamo ya kweli.

Ridhiwani alisema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuaga katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kabla ya maziko kwenye makaburi ya Kinondoni.

Ridhiwani alisema Rais Samia alishindwa kuhudhuria ibada hiyo kwa kuwa alikuwa na mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma.

Ridhiwani alisema Profesa Sarungi alikuwa ni mwanamapinduzi na atakumbukwa kwa kuwa kiunganishi cha watu.

Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba alisema Profesa Sarungi alibaki kuwa mwaminifu kwa nchi, mwenye maadili na hakuwa na unafiki.

Warioba alisema sifa zake huenda zikasaidia kizazi cha sasa na kijacho kikawa na juhudi, maarifa na jitihada kama alizokuwa nazo Sarungi.Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mara nyingi walikutana kujadili mambo mengi ikiwemo taaluma, makabila na aliwahi kumweleza kuwa wao si Wajaluo bali ni Wasuba. Pia alisema Sarungi aliwahi kumweleza udhaifu alionao hasa alipoingia katika siasa ilhali hakukulia kwenye siasa.

“Tumemsifia na duniani kote inajulikana kwamba ana shule ya sekondari kule kwao, ni rafiki yangu nilishapeleka vitabu kwenye shule yake, madaktari wa Muhimbili tuwaachie nyie wote mnataka tumkumbuke, tuwaombe wafanye taratibu na yeye ndiye aliyeanzisha MOI (Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili) jina lake lisipotee,” alisema Profesa Muhongo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button