Manispaa Geita yawahakikishia usalama wahitaji shuleni

HALMASHAURI ya Manispaa ya Geita imeweka wazi kuwa imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila shule inakuwa na miundombinu rafiki kwa watoto ambao ni wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rashid Muhaya ameeleza hayo katika hafla ya kupokea msaada viti mwendo, vifaa vya kujifunzia na michezo kutoka kampuni ya Isamilo.
Amesema ili kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia kwa makundi maalum halmashauri imesimamia kuhakikisha ujenzi wa miundombinu inayotoa mwanya rahisi kwa watoto hao kujifunza.

Amesema kwa kufuata muongozo wa elimu kila shule imejengewa vyoo na madarasa yenye miundombinu inayomwezesha mtoto mwenye mahitaji maalum kuingia na kutoka kwa urafiki.
Muhaya amekiri kuwa mbali na juhudi hizo bado kuna uhitaji wa vitabu vya watoto hususani kundi hilo maalum hvivo wadau wote wa maendeleo wanaombwa kuguswa kuwasaidia watoto hao.
“Tunatoa wito kwa wazazi wote pamoja na watoa taaluma kwamba watoto hawa wenye mahitaji maalum basi waingie shuleni ili wanufaike na haki yao moja kwa moja,” amesema.
Meneja wa Isamilo, Robison Mageta amesema msaada huo wa kundi maalum una thamani ya sh milioni tano ni sehemu ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Amesema CSR yao kwa mwisho wa mwaka 2025 imegusa zaidi kundi hilo lenye uhitaji mkubwa kwa kuwapa vifaa vitakavyowasaidia kukidhi mahitaji ya msingi kwenye sekta ya afya na elimu.
Mageta ametaja baadhi ya misaada waliyotoa ni pamoja na viti mwendo, vitabu na vifaa vya kutembelea pamoja na vitu vingine muhimu.
“Tunaomba pia wakandarasi wengine wenye makampuni kuendelea kushirikiana na serikali katika kufanikisha huduma bora kwa jamii hususani ya watu wenye mahitaji maalum,” amesema.



