Mamia wamiminika Tengeru kumzika Mtei

MAMIA ya waombolezaji wakiwamo viongozi wa serikali, vyama vya siasa, wakuu wa taasisi za kitaifa na kimataifa wameendelea kumiminika nyumbani kwa Mzee Edwin Mtei (93) eneo la Chama Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha kuomboleza na kusaini kitabu cha rambirambi.
Maziko ya Mtei ambaye ni mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mwenyekiti wa kwanza wa taifa anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake hapo. Alifariki dunia Januari 19, mwaka huu.

Miongoni mwa waliofika nyumbani kwake jana ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ambaye alisema uongozi, menejimenti na wafanyakazi wa BoT wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa, kwani Mtei alikuwa gavana wa kwanza Tanzania mwaka 1966 hadi 1974, na kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.
SOMA: Rais Samia amuomboleza Edwin Mtei
Tutuba alisema baada ya kupokea taarifa ya msiba, BoT ilishiriki moja kwa moja katika msiba huo kwa hali na mali kwa kushirikiana na familia, na hali hiyo itaenda hadi siku ya mwisho ya maziko ya Mzee Mtei.
Alisema BoT Makao Makuu Dar es Salaam ina maktaba maalumu yenye kuelezea jinsi alivyoitumikia benki hiyo kwa weledi, ikiwamo alivyobuni noti na sarafu ya kwanza nchini na kumkabidhi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Tuko hapa kama BoT kushiriki maombolezo na hatimaye maziko ya gavana wa kwanza wa benki hiyo nchini ambaye ameweka historia kubwa hapa nchini ya utendaji kazi ambao unaendelezwa hadi sasa,” alieleza Tutuba.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesikitishwa na taarifa zilizozagaa mitandaoni zikisema Chadema imetengwa katika msiba huo ikiwamo maziko ya leo, akisema taarifa hizo sio sahihi na zinapaswa kupuuzwa.
Mbowe alisema viongozi wa Chadema ngazi zote wapo Tengeru na wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na familia ya Mtei, toka kutangazwa kwa msiba na chama kimeshirikishwa kikamilifu.

Alisema katika maziko ya leo, viongozi mbalimbali wa serikali wilaya, mkoa, kitaifa na viongozi wa vyama vya siasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), taasisi za kitaifa na kimataifa, wamethibitisha kushiriki maziko hayo na watapewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi kumuenzi Mtei.
Mtei alizaliwa Julai 12, 1932 Marangu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, na aliasisi na kupewa usajili wa Chadema Januari 21, 1993. Kwa upande wake, mwanaharakati na mwandishi nguli nchini, Jenerali Ulimwengu amesema Mzee Mtei alijenga misingi imara ya thamani ya fedha ambayo imeweka uchumi wa nchi kuwa imara.
Ulimwengu alisema nyumbani kwa Mtei kuwa mchumi huyo alitengeneza misingi imara ya BoT iliyojenga thamani ya fedha ya Tanzania kuheshimika kitaifa na kimataifa, na ndio inayoheshimika kwa wakati wote hadi sasa.



