Maofisa habari serikalini waonywa utani na viongozi

MAOFISA Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali wametakiwa kuepuka kufanya utani na viongozi wao kwa kuwa itifaki inakataza jambo hilo.

Balozi Peter Kallaghe amesema hayo Dar es Salaam jana wakati wa kikao kazi cha 18 cha Maofisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali.

Balozi Kallaghe ametoa mada kuhusu itifaki ambazo maofisa habari wa serikali wanapaswa kuzizingatia katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Alisema si sahihi kwa maofisa hao kufanya utani au kuingilia mazungumzo ya utani na viongozi wao kwa kuwa itifaki hairuhusu jambo hilo.

Aliwataka maofisa hao wawashauri viongozi wao kuepuka mazungumzo ya utani na wasaidizi wao kwa kuwa wao ni viongozi na wanabeba alama ya nchi.

“Tuna wajibu wa kulinda heshima ya viongozi wetu na heshima ya nchi yetu, hivyo kazi yetu ni kuwasaidia viongozi wetu,” alisema Balozi Kallaghe aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu na Balozi wa Tanzania katika Uingereza.

Pia aliwakumbusha kuwa itifaki haitumiki tu kwa viongozi, bali hata kwa watu wengine wa kawaida, hivyo wanapaswa kuwahudumia kwa ustaarabu kwa kuwa itifaki ni ustaarabu.

Alipoulizwa kuhusu mantiki ya kuinama wanapopita mbele ya viongozi, alisema hiyo ni ishara ya kuomba radhi kutokana na dharura aliyonayo mtu wakati shughuli husika ikiendelea mbele ya mgeni rasmi.

Kuhusu namna ya kupanga ukaaji wa viongozi, Balozi Kallaghe aliwaeleza maofisa habari hao kuwa baada ya mgeni rasmi, kiongozi anayefuatia kwa wadhifa anatakiwa akae kulia kwa mgeni rasmi.

Hata hivyo, aliwataka wafanye kazi hiyo kwa kushirikiana na maofisa wenzao wa taasisi ambazo viongozi hao wanatoka ili kujua nyadhifa zao zilivyo.

Kwa kuwa Wimbo wa Taifa unapoimbwa kila mtu anapaswa kusimama kwa heshima na kwa kutulia, alisema jambo hilo haliwahusu wapigapicha maalumu walioandaliwa kupiga picha kwa lengo la kutunza historia ya tukio husika.

Mtaalamu wa mitandao ya kijamii, Mike Mushi, alisema siyo watu wote wanaofuatilia habari za taasisi husika wanaweza kuona maudhui yanayowekwa kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii, bali ni asilimia moja hadi sita tu ya watu ndiyo huona maudhui hayo.

Mushi alisema ili watu wote waone au wapate maudhui ambayo yanawekwa kwenye akaunti ya taasisi husika kwenye mtandao, hawana budi kulipia maudhui hayo.

Kutokana na changamoto ya usalama mitandaoni, aliwataka maofisa habari, uhusiano na mawasiliano kujua sera za taasisi zao zinasemaje kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii pamoja na kujua wadau wanaotaka kuwafikia na mbinu za kuwafikia.

Alitaja mambo mengine wanayopaswa kuyazingatia ni kuwa na misingi ya uendeshaji wa akaunti hizo za mitandao ya kijamii za taasisi zao ikiwamo kujua namna gani na wakati gani wa kujibu hoja za watu wanaofuatilia akaunti hizo na kujua linapotokea jambo la dharura kwenye akaunti hizo sera inawaelekeza wafanye nini.

 

Habari Zifananazo

Back to top button