Maofisa Waandamizi Jeshi la Polisi wajipanga kuimarisha amani

KILIMANJARO : MAOFISA Waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini wameazimia kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika katika hali ya amani, utulivu na usalama na kwamba hawatamuonea muhali mtu yeyote atakayejaribu kuvunja amani ya nchi.
Azimio hilo limefikiwa baada ya kukamilika kwa mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika kwa siku tano katika Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP) Camillus Wambura, Kamishna wa Intelijensi ya Jinai (CP) Charles Mkumbo amesema Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanapiga kura katika hali ya usalama na wamejipanga kudhibiti uhalifu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Aidha, alisema jeshi hilo lina jukumu kubwa la kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya usalama, amani na utulivu, hivyo katika kufikia azma hiyo limeazimia kusimamia sheria na kanuni zote za nchi, kulinda mikutano ya kisiasa ya vyama vyote na kuweka mazingira bora ya kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla.
Akifunga mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu alisisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kujipanga vizuri na kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu. SOMA: Polisi yaonya vitisho, uzushi Uchaguzi Mkuu
Aidha, alilihimiza jeshi hilo kuendelea kubaini viashiria vya uvunjifu wa amani na uchochezi kwenye mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi kwa kushirikiana na wadau wa teknolojia ya habari na mawasiliano kudhibiti makosa ya kimtandao. Akigusia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025, Gugu alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kwa umakini utekelezaji wa mikakati ya kiusalama kuelekea uchaguzi huo.



