Maonesho ya ujuzi, ajira kuwakutanisha vijana 3,000 Iringa

IRNGA: Zaidi ya vijana 3,000 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa wanatarajiwa kushiriki katika maonesho ya ujuzi, fani na ajira yatakayofanyika kuanzia Julai 25 hadi 27, mwaka huu, katika viwanja vya Mwembetogwa mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mratibu wa maonyesho hayo, Steven Mfuko, maandalizi yamefikia hatua za mwisho, huku lengo kuu likiwa ni kuwawezesha vijana kupata maarifa, fursa na msukumo wa kujenga maisha endelevu kupitia ajira, ujuzi wa ufundi na ujasiriamali.
“Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kijana: Ujuzi Wako, Fani Yako, Chaguo Lako’ ikihimiza vijana kutumia ujuzi walionao na kufanya maamuzi sahihi ya fani zao kwa maendeleo yao ya kiuchumi,” alisema Mfuko.
Alisema maonesho hayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ubalozi wa Uswisi nchini, Shirika la TIHub na Swisscontact kupitia Mradi wa SET.
Mfuko alieleza kuwa, miongoni mwa malengo ya maonyesho hayo ni kuongeza uelewa wa vijana kuhusu ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira, kuwaunganisha na waajiri na wataalamu wa sekta mbalimbali, pamoja na kuwaelimisha juu ya taasisi za kifedha na nafasi za ajira zilizopo kupitia mradi huo wa SET unaofadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi.
Alisema ufunguzi rasmi wa maonesho unatarajiwa kufanyika Jumamosi ya Julai 26, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa pamoja na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania.
Zaidi ya mabanda 50 yatakuwepo katika maonesho hayo, yakiwajumuisha waajiri, taasisi za mafunzo ya ujuzi, mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali, pamoja na taasisi za kifedha.
“Vijana watapata nafasi ya kujifunza kuhusu uandishi wa wasifu (CV), maandalizi ya usaili, uandishi wa miradi ya biashara, mahitaji ya kisheria ya kuanzisha biashara, na mbinu za kupata mitaji,” alibainisha Mfuko.
Kabla ya kuanza kwa maonyesho, kutafanyika kampeni ya siku nne ya uhamasishaji jamii kuanzia Julai 21 hadi 24.
Alisema kampeni hiyo itahusisha shughuli mbalimbali za kijamii kama uchangiaji damu, matangazo kupitia redio na televisheni, usafi katika stendi ya mabasi ya zamani, na uhamasishaji kwa kushirikiana na waendesha bodaboda.
Alisema Alhamisi ya Julai 24, Chuo Kikuu cha Iringa kitakuwa mwenyeji wa mdahalo maalum utakaowakutanisha wataalamu, wajasiriamali waliobobea na wawakilishi wa sekta binafsi, utalii na fedha.
Mada kuu ya mdahalo huo itakuwa “Fursa za Kiuchumi kwa Vijana Iringa,” na baadhi ya wazungumzaji watakuwa ni Said Hozza wa TaifaTek Ltd na Saida Yusufu Mgeni kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Mkoa wa Iringa.
“Maonyesho haya ni ya wazi kwa umma na hakuna kiingilio,” alisisitiza Mfuko huku akiwakaribisha vijana na wananchi wote kushiriki kikamilifu kwa manufaa ya maendeleo yao binafsi na kijamii.



