Mapambano ndoa, mimba za utotoni safari ya mafanikio Rukwa

JUHUDI katika kutoa elimu kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya kuendelea na masomo yao bila vikwazo zimewezesha mpango mkakati wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni ulioanzishwa miaka mitano iliyopita mkoani Rukwa kuleta mafanikio.

Shirika la Plan International limesema viashiria vinavyowaweka watoto wa kike katika hatari ya kuozwa au kupata mimba wakiwa chini ya miaka 18 vimeanza kupungua kwa kasi inayoridhisha mkoani humo.

Viashiria hivyo ni pamoja na umasikini, elimu duni, shinikizo rika, uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto na wanafunzi, ukatili na usawa wa kijinsia na idadi ndogo ya shule za bweni na zinazotoa chakula.

Advertisement

Vingine ni malezi hafifu, mila desturi na imani zinazomkandamiza mtoto wa kike, kuporomoka kwa maadili katika jamii, na kutowajibika kwa wazazi na viongozi katika ulinzi wa watoto wa kike.

Meneja wa Mradi wa Kupinga Mimba na Ndoa za Utotoni kupitia shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (Norad), Kisasu Sikalwanda anasema:

“Tulikuja Rukwa kusaidiana na serikali na wadau mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo, na wakati tukianza kutekeleza mradi huu hali ilikuwa mbaya.

Takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015 hadi 2016 zinaonesha asilimia 29 ya wanawake wenye miaka kati ya 15 na 19 mkoani humo walikuwa wajawazito au wamezaa.

Utafiti huo unaonesha katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2019 kulikuwa na jumla ya matukio 722 ya wanafunzi kupata mimba ambayo kati yake 171 yalitokea katika shule za msingi na 551 kwa shule za sekondari.

Sikalwanda aliyemaliza muda wake wa utumishi katika shirika hilo hivi karibuni anasema ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini, wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla umeleta mafanikio na kuwezesha watoto wa kike kupata haki zao za elimu, afya ya uzazi, na fursa za maisha bora.

Ofisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Fanikio Bitende anasema mimba za utotoni zimepungua kwa asilimia kubwa tangu kuanzishwa kwa mkakati huo mwaka 2019.

“Shule nyingi sasa zimeanzisha vikundi vya washauri rika ambavyo vimekuwa vikisaidia wasichana kujenga ujasiri wa kusema hapana kwa ngono zembe,” anaeleza Bitende.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Fanikio Bitende

Anasema takwimu katika shule zao za sekondari zinaonesha kupungua kwa mimba za utotoni kutoka 20 mwaka 2019/2020 hadi mimba sita mwaka 2022/2023.

Akitoa mfano wa Shule ya Sekondari Vuma, Bitende anasema idadi ya mimba ilipungua kutoka sita mwaka 2020 hadi sifuri mwaka 2023.

Katika shule ya Msingi Laela ‘A’ iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, ambako Leonard Mpasa ni mwalimu mkuu wake, elimu ya afya ya uzazi, ulinzi wa mtoto na makuzi kwa vijana hutolewa kila Jumatatu.

“Tumeweka mipango thabiti ya kuhakikisha wasichana wanapata uelewa kuhusu hedhi salama na namna ya kujilinda dhidi ya mimba na ndoa za utotoni,” anasema Mpasa.

Anasema kwa wasichana walio kwenye mabadiliko ya mwili, huduma za hedhi salama ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanaendelea kuhudhuria masomo.

Anashauri kuanzishwa kwa miradi ya kutengeneza taulo za kike ndani ya jamii ili kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje. Hii itawasaidia wasichana wengi kuendelea na masomo, na hivyo kupunguza hatari ya mimba za utotoni.

Akitoa takwimu za maafanikio na changamoto zilizopo anasema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shule hiyo imepiga hatua kubwa kitaaluma, huku kiwango cha ufaulu kikiongezeka hadi asilimia 97 kwa darasa la saba na hadi asilimia 100 kwa darasa la nne.

Aidha, katika shule hiyo yenye wanafunzi 1,464 ambao kati yake zaidi ya wanafunzi 800 ni wasichana, anasema hakuna kesi za mimba zilizoripotiwa, na utoro umepungua kwa kiasi kikubwa.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisalala Wiseman Cheyo, anaeleza kuwa elimu ya afya ya uzazi na makuzi kwa vijana imewasaidia wasichana wengi kujitambua katika kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni.

“Elimu hii imewezesha watoto wetu kuelewa miili yao na mabadiliko wanayopitia wanapoanza balehe-kama vile hedhi, ukuaji wa viungo vya uzazi na mabadiliko ya kihisia, lakini pia imewawezesha kujua haki zao za kiafya na kijinsia ikiwemo haki ya kujiepusha na ndoa za kulazimishwa na kujilinda dhidi ya vishawishi vya mapema,” anasema.

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Laela A, Leonard Mpasa

Mwalimu Cheyo anasema elimu hiyo imewawezesha pia watoto kujiamini na kujiepusha na makundi hatarishi pamoja na kufahamu njia za kujikinga na mimba, na kujua madhara ya mimba za utotoni.

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Sumbawanga, Patricia James, anasema takwimu za mwaka 2022 na 202 zinaonesha mimba katika shule za msingi zimepungua kutoka nane hadi tatu, na kati ya mwaka 2023 na Juni 2024 kulikuwa na tukio moja tu la mimba.

Anasisitiza kuwa mradi huo unapaswa kuenea katika shule zote ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanalindwa dhidi ya changamoto hizo.

Mratibu wa Shirika la YES Tanzania lililoshirikiana na Plan International kutekeleza mradi huo, Shabani Ramadhani, anasema katika shule ya msingi Itindi wilayani Nkasi, walimu wameona mabadiliko makubwa ambapo utoro wa wasichana umepungua kwa zaidi ya asilimia 70.

“Programu za kielimu na za afya zimeonesha kuwa na uwezo wa kubadilisha maisha ya watoto wa kike katika jamii hizi. Mafanikio yaliyopatikana mkoani Rukwa yanaweza kutumika kama mfano mzuri wa kile kinachoweza kufanywa kitaifa na kimataifa ili kumaliza tatizo hili,” anasema Ramadhani.

Lidia Wampembe, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Itindi, anaeleza namna ambavyo elimu hiyo imemsaidia kukabiliana na vishawishi vya mimba za utotoni, licha ya changamoto za mazingira ya shule.

“Sasa najua namna ya kujilinda, na nina malengo ya kuendelea na masomo yangu hadi chuo kikuu,” anasema Lidia.

Hata hivyo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Donald Nsoko anasema; “Licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna mila na desturi zinazowaweka watoto wa kike katika hatari ya kuozwa au kupata mimba, na jamii nyingi bado hazijafikia uelewa kamili wa sheria zinazosimamia haki za watoto.”

Chifu wa Wafipa, Chifu Malema Sinyangwe anasema; “Tukifuata na kuzilinda mila na desturi zetu tatizo la ongezeko la ndoa na mimba za utotoni ambalo ni moja ya changamoto ya kiafya kwa vijana wetu wa kike-litakwisha.”

Chifu Malema anasema mimba za utotoni hazikubaliki katika jamii ya wana Rukwa na ndio maana mila na desturi zinawataka wazee kwa kupitia madarasa ya kimila wawaangalie watoto wanaokaribia balahe na kuwafunda.

Anasema mtoto kike akishakaribia kuvunja ungo, mama anawajibika kuchunga nyendo zake, kutomruhusu kushirikiana na mabinti watukutu, na urafiki wa karibu na wavulana nje ya mambo yanayowahusu kama vijana wa rika moja na kumtahadharisha yanayoweza kumpata iwapo hatazingatia kanuni za kuishi katika hali ya kupevuka mwili.

“Tunataka elimu, mila na desturi na sheria za nchi ziifanye jamii ichukizwe na vitendo vya watoto wao wa kike kuwa na mahusiano ya kingono ambayo wanaamini yatawaharibu mabinti kwa kuwasababishia ujauzito na matatizo mengine ya kiafya,” anasema.

Kuhusu jukumu la serikali na uboreshaji wa sheria; Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Elimu ya mwaka 2016 zimetajwa kama nguzo muhimu katika kupambana na mimba na ndoa za utotoni.

Viongozi wa dini nao wamekuwa na jukumu kubwa katika kutoa mafunzo ya kidini yanayolenga kuhimiza jamii kulinda haki za watoto wa kike mkoani Rukwa.

Wamepaza sauti wakitaka kujua ni lini serikali itaifanyia mabadiliko Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 waliyosema mapungufu na changamoto zake zinachochea mimba na ndoa za utotoni mkoani mwao na Taifa kwa ujumla.

Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali, anaeleza kuwa mabaraza ya dini yamekuwa yakitoa elimu kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni na kuhimiza wazazi kuwaendeleza watoto wa kike kielimu.

“Sheria ya sasa inamtaka mwanaume kuoa akiwa na umri wa miaka 18 ambao kikatiba ni mtu mzima, lakini sheria hiyo hiyo inaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa hajafikia utu uzima,” anasema Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Rukwa.

Padri Charles Kasuku wa Jimbo Katoliki Sumbawanga anasema muongozo wa jumla wa dini unapinga ndoa za utotoni na kukataza matendo yote ya uzinzi hivyo ni muhimu serikali kupitia bunge lake ikawa na sheria ya ndoa ambayo haikinzani na sheria ya mtoto na haki zake zingine.

Mchungaji Emmanuel Sikazwe wa Kanisa la Morovian Sumbawanga anakumbusha jinsi Sheria ya Ndoa inavyokinzana pia na kanuni za adhabu ambayo imeanisha kwamba ni kosa la ubakaji kwa mtu yoyote kufanya ngono na mtoto chini ya miaka 18 isipokua kama ameolewa.

Mei, mwaka huu Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amenukuliwa bungeni akisema serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imekamilisha uandaaji wa muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kwamba taratibu zinaandaliwa za kuufikisha Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa kisha kupitishwa kuwa sheria kamili.

Sagini anasema serikali ilianza maandalizi ya muswada huo baada ya kukusanya maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo wazee wa kimila, viongozi wa kidini, wanataaluma, wanafunzi wa ngazi mbalimbali, watu mashuhuri na waheshimiwa wabunge juu ya maboresho ya sheria hiyo kuhusu kuondoa mabishano ya umri upi kwa sasa uwe wa kuoa au kuolewa.

Wakati Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) za mwaka 2017 zinaonesha Tanzania ni ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashiriki kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudani Kusini na Uganda.

Takwimu za Unicef zinaonesha kiwango cha watoto wanaoozwa wakiwa na umri chini ya miaka 18 nchini Tanzania ni asilimia 31, Sudani Kusini ina asilimia 52 na Uganda asilimia 40.

Huko Kenya, Sheria ya Ndoa Namba 4 ya mwaka 2014 ya nchi hiyo inasema ili kuoa au kuolewa utahitaji kuwa na umri wa miaka 18 au zaidi na si vinginevyo.