Mapambano ya VVU Kagera yaingia awamu mpya

KAGERA: WIZARA ya Afya imeitambulisha rasmi taasisi ya kimataifa ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) kuwa mdau mpya wa kuratibu na kuendeleza afua za VVU na UKIMWI mkoani Kagera na mikoa mingine saba.

Hatua hiyo ni kufuatia kumalizika kwa shughuli za uratibu zilizokuwa zikitekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Management and Development for Health (MDH) tangu Septemba 2026.

MDH ilitekeleza shughuli hizo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kipindi cha miaka 13, huku ujio wa EGPAF ukilenga kuendeleza juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi hivyo.

Mkurugenzi Mkazi wa EGPAF, Dk Sajida Kimambo, alisema taasisi hiyo ina mkakati wa kuchangia kufikiwa kwa malengo ya kimataifa ya 95-95-95 ifikapo mwaka 2030, hususan kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanapata huduma za matibabu na kufikia hatua ya kufubaza virusi.

Alisema moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo ni kuimarisha huduma kwa wanawake wajawazito ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.

Alieleza kuwa lengo ni kuhakikisha watoto wanazaliwa na kukua bila kuambukizwa VVU kutoka kwa mama zao, hatua itakayosaidia kulinda afya za watoto na kupunguza maambukizi mapya katika jamii.

Aidha, alisema mradi huo utajikita pia katika makundi ya vijana balehe kwa kuimarisha elimu, uelewa na upatikanaji wa huduma zinazohusiana na kinga na matibabu ya VVU na UKIMWI.

Dk Kimambo alibainisha kuwa mabadiliko muhimu katika mfumo wa utekelezaji wa mradi huo ni matumizi ya utaratibu wa ufadhili unaozingatia matokeo ya kazi, ambapo malipo ya fedha za wafadhili yatahusishwa na matokeo yaliyofikiwa, tofauti na baadhi ya mifumo iliyotumika katika miradi iliyotangulia.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bwai Biseko, alisema mkoa uko tayari kushirikiana na EGPAF katika kuendeleza afua za VVU na UKIMWI na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma zinazohitajika.

Hata hivyo, aliiomba taasisi hiyo na wafadhili kuzingatia vijana waliopata mafunzo na kushiriki katika kutoa huduma kwa wagonjwa kupitia miradi iliyokuwa ikitekelezwa na MDH.

Alisema baadhi ya vijana hao wamekata tamaa baada ya shughuli za shirika hilo kumalizika, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi ya kuendelea kutumia ujuzi na uzoefu walioupata katika huduma za afya.

Dk Anath Rwebembela, Mshauri wa Programu wa Wizara ya Afya, alisema mradi huo unatarajiwa kufadhiliwa na Serikali ya Marekani kwa kipindi cha mwaka mmoja, hatua itakayowezesha kupima utekelezaji wake na matokeo yatakayopatikana ili kuangalia uwezekano wa kuongeza mkataba na kufikia mwaka 2030.

Alisema EGPAF imekuwa nchini Tanzania kwa muda mrefu na imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali na EGPAF unatarajiwa kuendeleza juhudi za kuzuia maambukizi mapya ya VVU, kuimarisha huduma kwa watu wanaoishi na virusi hivyo na kuwalinda watoto pamoja na vijana dhidi ya maambukizi.

Aidha, utambulisho wa EGPAF uliwakutanisha Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Halmashauri, Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya, Mganga Mkuu wa Mkoa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya mdau huyo mpya na mwelekeo wa utekelezaji wa mradi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button