Maparawe kwa raha zao maji safi

MTWARA; WANANCHI wa Kijiji cha Maparawe, wilayani Masasi, mkoani Mtwara wameshangilia kupata mradi wa kwanza wa maji safi na salama ambao utawaepusha kwenda mto Ruvuma kukumbana na adha ya kuliwa na mamba, kujeruhiwa na wengine kupoteza viungo vya miili.
Wakizungumza na mwaandishi wa habari hizi kijijini hapo, wakazi hao wamesema mradi huo wa kisima sasa utabadilisha historia ya upatikanaji wa maji ya kupambana na mamba wakati wakichota maji.
“Kijiji hiki kwa muda mrefu tumekuwa na changamoto ya maji, mto Ruvuma ambao umejaa mamba ndio ulikuwa tegemeo kwetu kwa huduma zote za maji ikiwemo kunywa, tulikuwa hatuna sehemu ya kupata maji na unavyojua maji ni uhai tulilazimika kwenda kuyafuata licha ya kukumbana na mamba , wengine wakiliwa , kujeruhiwa na hata kupoteza viungo vya miili yetu,” amesema Mzee Selaman Msera.
Halima Jaffar amesema ujenzi wa mradi wa maji kwenye kijiji hicho ni hatua kubwa kuwakomboa wanawake na wasichana ambao wengi wao waliathirika zaidi wakati wa kupata maji mto Ruvuma.
Mwenyeki wa Kijiji hicho Afat Sadiki, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya jambo kubwa sana kuwaletea kisima cha maji na kubadilisha historia, huku akisema watapumzika vilio vya mara kwa mara kutokana na mamba kujeruhi watu lakini pia kutulia na kuanza kufanya shughuli za maendeleo ambazo pia tiliathirika.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Juma Yahya amesema kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji kumi katika wilaya ya Masasi, ambavyo vinanufaika na programu maalumu ya uchimbaji wa visima 900 nchi nzima.



