Mapato, makusanyo yapaa TIC

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema mapato na makusanyo yake kwa mwezi yamefikia Sh bilioni moja kutoka milioni 400 iliyokuwa inakusanya 2022.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema kuongezeka kwa mapato hayo kunatokana na mabadiliko ya sheria yaliyowezesha kuongeza wawekezaji kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi.

Teri alisema hayo Dodoma jana wakati akieleza mafanikio ya kituo hicho ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Serikali ya Rais Samia kwa miaka minne iliyopita imefanya maboresho ya sheria ambazo zinalenga kuleta urahisi, ufanishi, zinazowapa kipaumbele Watanzania kupunguza urasimu na kuwathamnini wawekezaji wanaokuja na waliopo,” alisema.

Teri alisema kituo hicho kimefanya maboresho katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji kwa urahisi na ufanisi na kinatoa mafunzo kwa watumishi wake ili wawahudumie wawekezaji kwa ufanisi mkubwa.

Pia, alisema TIC imeandaa dirisha linalotoa huduma za taasisi 16 zinazohusika katika masuala ya kuanzisha uwekezaji ili kumrahisishia mwekezaji katika kupata huduma.

“Tuna dirisha la pamoja linakutanisha taasisi 16 za serikali kwamba ukija TIC huna haja ya kwenda TRA kupata TIN namba, NIDA kupata kitambulisho. Taasisi zote 16 zinazohusika na uanzishwaji na uendeshaji wa biashara mpaka NEMC wote tupo nao ndani ya kituo cha uwekezaji na huduma zote zinapatikana pale,” alifafanua Teri.

Aliongeza: “Tumewekeza katika mifumo ya Tehama kwa sasa maombi ya kuwa mwekezaji unaileta katika mtandao, inapitiwa katika mtandao na inakubaliwa katika mtandao bila kufika katika ofisi”.

Aidha, Teri amezitaja ziara za Rais Samia nje ya nchi na diplomasia imara ya kiuchumi kama moja ya kichocheo katika kuongeza wawekezaji nchini.

“Ametembelea Marekani, China, Korea Kusini, Falme za Kiarabu, Jumuiya ya Ulaya, ni nchi ambazo zina mitaji mikubwa zina wawekezaji ambao wanataka na kwenda kuzalisha bidhaa zao nchi nyingine,” alisema bosi wa TIC.

Amepongeza mchango wa mabalozi na wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi kwa jitihada zao katika kuvutia wawekezaji.

“Mnaona kwenye mitandao mikutano ya mitandaoni na mikutano ya moja kwa moja ambayo viongozi wetu mabalozi ambao ni wawakilishi wa rais na nchi yetu nje wanafanya ili kuvutia na kueleza fursa zilizopo Tanzania na kuwaleta nchini kwetu,” alifafanua Teri.

Aidha, alisema katika miaka minne ya uongozi wa awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la wastani wa uwekezaji nchini kutoka miradi 256 mwaka 2021 hadi 901 mwaka 2024 na kufanya jumla ya miradi iliyosajiliwa toka 2021 hadi 2024 kuwa 2,020 ambayo ni ongezeko la asilimia 91.

Pia, amesema katika uwekezaji ndani ya miaka minne mitaji imeongezeka huku malengo yao yakiwa ni kufikia mitaji ya dola bilioni 15 ndani ya mwaka huu.

*Imeandikwa na Magnus Mahenge (Dodoma) na Shakila Mtambo (Dar)

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button