Mapya yaibuka mwanafunzi aliyebadilishiwa namba ya mtihani

Mapya yaibuka mwanafunzi aliyebadilishiwa namba ya mtihani

SERIKALI imetangaza kuifungia shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani kwa muda usiojulikana.

Shule hiyo imefungiwa kutokana na taarifa ya Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani pamoja na taarifa ya Wataalam wa Miandiko (Forensic Bureau), kutoka Jeshi la Polisi nchini kubaini kuwa jumla ya watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo PS1408009 shule ya awali na Msingi Chalinze Modern Islamic.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 25,2022,  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,  amesema shule hiyo imefungiwa kwa mujibu wa kifungu cha 4(8) cha kanuni za mitihani 2016.

Advertisement

Hatua ya kuifungia shule hiyo imekuja siku  chache baada ya mwanafunzi Iptisam Suleiman Slim, video yake kusambaa kwenye mitandao akilalamikia kubadilishiwa namba ya mtihani, jambo ambalo kamati uchunguzi umebaini ni kweli.

Kufuatia hali hiyo, serikali imefanya uchunguzi kupitia kwa wataalamu wa miandiko katika skripti za watahiniwa, umebaini kuwa mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0033 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0034 katika somo la sita, ambalo ni la mwisho.

Amesema pia mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0034 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0033 katika somo la sita, huku mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0040 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0039 katika somo la sita .

“Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0039 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0043 katika somo la sita.

“Vilevile, mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0041 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0040 katika somo la sita na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0042 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0041 katika somo la sita.

“Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0043 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0042 katika somo la sita,” amesema Waziri Mkenda.

Amesema kuwa dosari iliyojitokeza katika namba za watahiniwa hao, ilisababishwa na uzembe wa watumishi wanne ambao ni Muddy Elphas Mndeme, msimamizi wa mkondo, Vitalisa Lucas Kindole, msimamizi mkuu, Amran Bakari Ramadhani, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo na Rajab Omary Kijangwa ambae ni mwalimu wa takwimu.

Waziri Mkenda amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani, umebaini kuwa Mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim alifanya masomo matano kwa kutumia namba PS1408009/0040 na somo la sita kwa kutumia namba PS1408009/0039.

Amesema Watahiniwa wengine wanne pia walibadilishiwa namba katika somo la sita, ambapo Jasmin Abdallah Mzee alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0041 na somo la sita kwa kutumia namba PS1408009/0040.

Jokha Abubakar Nassor alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0042 na somo la sita kwa kutumia namba PS1408009/0041 na Khailat Hamis Mohamed alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0043 na somo la sita kwa kutumia namba PS1408009/0042.

Prof Mkenda amesema Khaula Khamis Mruma alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0039 na somo la sita kwa kutumia namba PS1408009/0043.

Waziri Mkenda amesema uchunguzi huo umefanywa kufuatia tukio la Oktoba 13, ambapo taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya awali na msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika tarehe Oktoba 5 na 6, 2022.

Waziri Mkenda amempongeza mwanafunzi Iptisam, kwa kutambua na kupigania haki yake na wanafunzi wenzake na kusisitiza kuwa shule yoyote itakayobainika kufanya vitendo vya udanganyifu wa mitihani, itafungiwa na hata kufutwa kabisa kuendesha shughuli za elimu nchini.

/* */