ZANZIBAR: HATIMAE Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin Amour Juma kwa mara ya kwanza ameonekana adharani baada ya miaka kadhaa huku akitaka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukisimamia vyema chama hicho huku wakionya usiri wa vikao vya chama lazima uzingatiwe.
Rais Salmin maarufu ‘Komandoo’ametoa kauli hiyo leo Machi 25, 2024 alipotembelewa na Katibu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye amewatembelea Marais Wastaafu akiwemo Dk. Ali Mohamed Shein, kwa nyakati tofauti katika makazi yao, pamoja na Wazee wa CCM kwenye mikutano yao ya mabaraza, Pemba na Zanzibar.
Akizungumza Dk Salmin amesema amefarijika kutembelewa na Katibu huyo wa CCM Bara na kusema ““Asanteni. Waambie pia nawasalimia. Simamieni Chama…chama kijengwe, kisimamiwe kupata ushindi mzuri.”
Kwa upande wa Dk. Shein, amesisitiza umuhimu wa CCM kuendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake.
“CCM ni chama makini sana. Kina misingi na taratibu zake. Na jambo zuri ni kwamba Katibu Mkuu ndiye msimamizi. Nakujua, tumekuwa wote Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa muda mrefu.
“Sina shaka nawe kuyasimamia haya. Tukipindisha taratibu tutaanza kwenda kombo. Jengine ni suala la usiri wa vikao, lazima vikao viwe na siri,” amesema Dk. Shein.
Kwa upande wake, Balozi Nchimbi amesema shauri na maelekezo ya viongozi Wastaafu wa Chama na Serikali, pamoja na Wazee wa CCM kuhusu umuhimu wa kuendelea kukiimarisha Chama, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatumikia watu vizuri, yatafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.