Marekani haitaiacha NATO – Rutte

UHOLANZI: KATIBU Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte, amesema ana uhakika kuwa Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda wanachama wa jumuiya hiyo iwapo watashambuliwa.
Akizungumza mjini The Hague kabla ya mkutano wa kilele wa NATO, Rutte alisema anaamini Marekani bado imejitoa kwa dhati kulinda usalama wa wanachama wa NATO kupitia Ibara ya Tano ya mkataba wa jumuiya hiyo, ambayo inataja kuwa shambulio dhidi ya nchi moja ni sawa na kushambulia zote.
“Kwangu mimi ni wazi kabisa kuwa Marekani imejitolea kikamilifu kwa NATO. Tunapaswa kuimarisha ulinzi wetu dhidi ya Urusi na vitisho vingine, sambamba na kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu wa kifedha katika bajeti ya pamoja,” alisema Rutte.
Hata hivyo, wasiwasi umeibuka kutoka kwa baadhi ya wachambuzi wa kimataifa kuhusu msimamo wa Rais Trump, hasa kutokana na kauli zake za awali zinazopinga mzigo mkubwa wa kifedha ambao Marekani hubeba ndani ya jumuiya hiyo.
Trump naye alizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuwasili katika mkutano huo, ambapo alisisitiza kuwa Ibara ya Tano ina vipengele vingi vya kuzingatia, lakini akasisitiza kuwa ataendelea kujitolea kulinda maisha ya watu.
SOMA: Finland kujiunga Nato



