Mary Rusimbi; aliacha ‘ajira nono’ kuongoza TGNP

JANA gazeti hili lilikuwa na makala iliyoeleza wasifu wa Mkurugenzi Mstaafu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT-Tanzania), Mary Rusimbi na namna anavyoelezea asili ya harakati za kijinsia, uongozi na alivyoamua kuanzisha kituo cha ‘kutibu’ wanawake kihisia na kisaikolojia.

Leo mwandishi Stella Nyemenohi anaangazia harakati zake kupitia taasisi lukuki alizoongoza. Fuatilia
“Nilibahatika kuwa kati ya waliosoma wakati huo, Tanzania chini ya falsafa ya Nyerere ya ushiriki wa watu wote katika demokrasia,” anaanza kueleza safari yake ya elimu, ajira na ushiriki wa harakati za kijinsia
Anasema walifundishwa kwamba uzalendo ni njia mojawapo ya kukuza demokrasia ya nchi.

Baada ya kuhitimu kidato cha sita, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1973 na baada ya mahafali ya kuhitimu Septemba 1976, kesho yake walipangiwa ajira katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dar es Salaam.
Mwenyewe anasema huko alijifunza mengi na kuchangia kuleta ushiriki wa kidemokrasia.

Advertisement

“Tulikuwa tukifundisha wanawake na wanaume lakini zaidi… usipompa maarifa mwanamke maana yake unamtoa katika ushiriki wa demokrasia.”Baadaye alijiendeleza katika masuala ya elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii.

“Nikajikuta naingizwa na maarifa na uelewa mpana wa ushiriki wa jamii katika maendeleo yao,” anasema.

Anasema aliporudi akiwa na digrii ya pili aliyoipata New Zealand kati ya mwaka 1981-1983, ilimwongezea nguvu na maarifa katika eneo la maendeleo ya jamii.

Akiwa katika taasisi hiyo na wenzake, walianzisha kitengo cha elimu na wanawake huku akiendelea kufundisha katika taasisi hiyo.

Kupitia kikundi hicho, walikuwa wakikutana kuzungumza, kusaidiana na hata masuala mengine wakiyapeleka kwenye ngazi husika za uongozi.

“Nakumbuka tulifanya utafiti na wenzetu wengine waliotoka nje na chuo chetu, serikali ilisapoti,” anakumbuka walivyokwenda maeneo ya vijijini.

AJIRA UBALOZINI

Baada ya miaka 12 ya kufundisha katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Rusimbi anasema Chuo cha Sussex cha Uingereza kilitangaza kozi fupi kuhusu jinsia na maendeleo.

“Ilikuwa ni kozi ya cheti, tukaenda wanawake watatu. Kilichotusaidia tukawa na nguvu, ni uzoefu tuliotoka nao huku maana kozi yoyote inatakiwa ikutane na uzoefu wako,” anasema.

Kwa mujibu wa Rusimbi, uzoefu huo si ndani ya taasisi pekee, bali pia nje ya ofisi hususan alipokuwa anakutana na mwanaharakati maarufu wa masuala ya jinsia na maendeleo, Profesa Marjorie Mbilinyi.

Anasema waliporudi nchini, walikuwa ‘wameiva’ kutokana na elimu ya usawa wa jinsia na si usawa wa kukwaruzana wanawake na wanaume au kugombana gombana.

Rusimbi anakiri kuwa, walielimishwa usawa na misingi yake kupitia kozi hiyo wakielezwa kwamba jinsia ina wanawake na wanaume ikichambua ni nani wanakosa rasilimali muhimu.

“Kusema kweli tulirudi na ‘zana’. Ilikuwa mwaka 1987/88. Haikuwa kozi ya muda mrefu, lakini ilikuwa nzuri na ilitusaidia sana kurudi na uelewa wa uchambuzi. Mimi kule nikajikita kwenye masuala ya jinsia na sera,” anasema.

Anaeleza kwamba kwa kuwa katika Taasisi ya Watu Wazima alikuwa akifundisha masuala ya sera na elimu ya watu wazima na kwamba, kozi hiyo ilimpa nguvu ya uelewa wa sera.

Alipata uelewa wa sera zinavyofanya kazi, zinavyotengenezwa na umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kuingiza sauti zao.

Baada ya kutoka kwenye kozi hiyo fupi, hakuendelea kukaa katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Anasema, “Baada ya kozi, nilikaa muda mfupi katika taasisi (takribani miaka miwili). Tulianza kutafutwa na balozi mbalimbali kwa sababu kilikuwa kipindi ambacho masuala ya wanawake na maendeleo yalishika kasi.”

Anasema kilikuwa kipindi cha hamasa ya Wanawake Katika Maendeleo (WID) kulingana na sera za kimataifa na mikutano mingi huku baadhi ya wanawake hususan, Getrude Mongella wakishiriki.

“Na sisi tulikuwa tukiwaangalia, nikashiriki kidogo kidogo. Kwa hiyo kulikuwa na huo mwamko wa kusema hebu tuingize masuala ya wanawake zaidi katika maendeleo.”

“Baadaye watu wakasema mbona tayari wanawake wako kwenye maendeleo? Mbona mwanamke ni mkulima na mwanaume ni mkulima unasemaje tumuingize kwenye maendeleo? Kwa hiyo hilo wazo la wanawake na maendeleo likafifia. Ikaja suala la jinsia na maendeleo.”

Kukawepo msimamo wa kuangalia sheria na sera kama zinaingiza hayo masuala. Anasema elimu ndogo ya masuala ya jinsia ilifanya achukuliwe na ubalozi wa Canada nchini Tanzania.

Aliunganisha nguvu ya harakati za jinsia na maendeleo, ikizingatiwa kwamba ubalozi ulikuwa umeanzisha programu hizo za jinsia.

Akapewa cheo cha Ofisa Mipango ya Jinsia (wa Tanzania) na kazi yake ikiwa ni kushauri ubalozi kuhusu masuala ya jinsia.

Anasema kilikuwa kipindi ambacho balozi zilikuwa zinashika fedha. Ndipo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yalianza kuibuka kidogo kidogo.

Miongoni mwa kazi alizofanya, anasema ni pamoja na kwenda na ubalozi kwenye majadiliano na serikali kuhusu masuala ya jinsia.

Ubalozi wa Canada ulipofungwa (wakati huo), alihamia katika Ubalozi wa Uholanzi ambako miongoni mwa kazi zake kubwa ilikuwa ni kutazama NGOs na kuzisaidia kifedha. Alifanya kazi katika balozi kwa miaka 12.

VUGUVUGU LA BEIJING

Rusimbi anasimulia vuguvugu la Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake uliofanyika Beijing, China 1995 na ushiriki wake.

Anasema ni mkutano ulioleta mabadiliko makubwa miongoni mwa wanawake. Ulisimama kidete kudai na kutetea haki za msingi za wanawake.

Anasema ubalozini kulikuwa na fungu kubwa la kusaidia wanawake waliokwenda kupeleka ajenda ya Tanzania.
“Ushiriki wa wanawake kama sisi… Tulifanya ushiriki mkubwa sana kitaifa. Kwa mfano, tulitengeneza ajenda na ajenda hazikutengenezwa kwa kukalishwa hoteli kama hapa Dar es Salaam bali tulikwenda vijijini,” anasema.

Anasimulia zaidi, “Kulikuwa na kamati kadhaa zilizotengenezwa kwenda vijijini kusikiliza ajenda za wanawake na kuelezea umuhimu wa mkutano wa Beijing.

… Kwamba serikali zote zikae chini, zikubaliane hili suala la usawa wa kijinsia, litaingizwa vizuri kwenye mikakati yake mpaka kwenye bajeti.”

Kwa mujibu wa Rusimbi, ushiriki wake katika mkutano wa Beijing ulikuwa kupitia ubalozini uliopeleka fedha kwa asasi mbalimbali, kazi iliyofanywa nae katika eneo lake.

ITAENDELEA…