Mashindano ya magari Asas kufanyika tena mwakani

KAMPUNI ya Asas imenogewa na mashindano ya magari Afrika (Africa Rally Championship) na mashindano ya magari ya taifa (Asas National Rally Championship) ikiahidi kuyaleta tena mwakani mkoani Iringa kwa udhamini utakayoyafanya yawe bora zaidi.

Siku ya kwanza ya fainali za mwaka huu imefanyika jana katika shamba la Asas la Matembo wilayani Iringa na siku ya pili na ya mwisho kwa mwaka huu itatimua vumbi leo katika shamba la miti la Saohili wilayani Mufindi.

Pamoja na gari yake kupata hitilafu siku ya kwanza huku moja ya tairi za gari yake aina ya Ford Fiesta Proto ikipata pancha na kumpotezea muda, mshiriki maarufu wa mashindano ya magari ya taifa, Ahamed Huwel ameahidi kumaliza akiwa kinara.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kumaliza siku ya kwanza ya fainali ya mashindano hayo, Huwel ameipongeza kampuni ya Asas kwa udhamini wa mashindano hayo akisema wamayaongezea chachu na ubora huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kuyaunga mkono.

Amesema Tanzania inaweza kutoa mshindi wa Afrika kama zilivyo nchi jirani za Kenya na Uganda kama itayaongezea uwekezaji kwani inao madereva wazuri wanaoweza kushindana ipasavyo.

Naye Karan Patel wa timu ya KCB Kenya amesema shauku yake ni kuona anaibuka kidedea katika mashindano hayo kwa upande wa Afrika.

“Umekuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwetu, ni matarajio yetu tutamaliza mashindano haya ya Afrika yanayofanyika sambamba na mashindano ya Taifa tukiwa mabingwa. Lengo letu sio kushinda tu, lengo letu ni kukusanya alama nyingi zitakazotuwezesha kushinda,” Patel amesema.

Mmoja wa wakurugenzi wa makampuni ya Asas, Ahamed Asas amesema; “Tumewiwa kudhamini mashindano haya kwa mara nyingine tena mwakani. Tutayaleta tena Iringa na tuyahakikisha tunafanya kila linalowezekana ili yawe bora zaidi.”

Akizungumzia umuhimu na manufaa ya mashindano hayo Asas amesema ni kichocheo cha uwekezaji na utalii kwani yanavutia wageni wa ndani na nje, yanaongeza mapato ya mkoa na watu wake na hivyo kuboresha maendeleo ya kiuchumi katika eneo husika.

Naye Afisa Utalii wa Shamba la Miti la Saohill, Bob Matunda amesema siku ya pili ya fainali ya mashindano hayo inafanyika katika shamba hilo kama moja ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan katika kutunza mazingira kwa kuhamasisha upandaji wa miti.

“Lakini pia wageni wote watakaokuja wanaweza kufanya utalii wa mazingira kwasababu shamba lina njia katika miti ya kupanda na ya asili yenye mandhari nzuri, maeneo yanayoweza kutumika pia kwa uwekezaji wa kitalii,” amesema.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x