Mashindano ya riadha Utu Kwanza yaja

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Utu Kwanza, limeandaa mbio ziitwazo Utu Kwanza Run kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasaidia wananchi mbalimbali walio katika nafasi finyu ya kupata huduma ya msaada wa kisheria, ikiwemo huduma ya kwanza ya kisheria hususan kwa wale walioko magerezani na mahakamani pamoja na familia zao.

Akizungumza leo Agosti 10, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa shirika hilo Wakili Shehzada Walli, amesema, mbio hizo zinatatajiwa kufanyika Septemba 10, 2023 jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Leaders Klabu, na kutoa wito wito kwa kila mmoja kuunga mkono Utu Kwanza Run katika kufanikisha mbio hizo.

“Ili kuweza kufanikisha tuliyoazimia kama taasisi ya Utu Kwanza ikiwemo kutoa msaada wa kisheria pamoja na huduma ya kwanza ya kisheria (first response) kuwasaidia wananchi mbalimbali hususan walioko mahakamani, tumeamua kuja na mbio maalum zinazoitwa Utu Kwanza Run kwa lengo la kuchangisha fedha ili kufanikisha azma hiyo ,” amesema Wakili Walli na kuongeza:

Advertisement

“Utu Kwanza Run itafanyika Septemba 10, 2023 ambapo katika siku hiyo kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8 mchana kutakuwa na dawati la kutoa msaada wa kisheria hususan wale walioko magerezani. Tunawaomba familia zao waweze kujumuika nasi siku hii.”

Akielezea mpangilio wa mbio hizo, Wakili Walli amesema, kutakuwa na kilometa 5 na 10 hadi kilometa 60 kwa wanaokimbia na kutembea, kwa upande wa waendesha baiskeli itakuwa ni kilometa 25 hadi kilometa 60 .

Wakili Walli ameeleza kuwa huduma ya kwanza ya msaada wa kisheria na msaada wa kisheria kwa ujumla watakaoutoa itatolewa kwa kuanzia katika Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya na kubainisha kuwa katika mahakama hizo wengi wao wako katika nafasi finyu sana ya kupata msaada wa kisheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Akili Masawe, amelipongeza shirika hilo kwa kuja na ubunifu katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ikiwemo kuja na mbinu tofauti.

“Kitu wanachokwenda kukifanya taasisi ya Utu Kwanza kutoa huduma ya kwanza ya msaada wa kisheria ni cha kipekee na cha kupongeza, kitu ambacho ni tofauti na wadau wengine wanaotoa msaada wa kisheria kwani wamewekeza katika makosa ya jinai, na jambo hili limekuja katika muda mwafaka wa mabadiliko ya mfumo wa haki jinai,” amesema Akili Masawe.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Moil Altaf Mansoor amesema, hatua ya taasisi ya Utu Kwanza kuanzisha mradi wa Dawati la Msaada wa Kisheria (Legal Aid Desk Project), inalenga katika kuhakikisha utu na haki ya mtu inapatikana na ni miongoni mwa jambo muhimu sana kwa nchi.

“Tunahitajika kuunga mkono hatua za kupatikana haki na utu, kwa kuwa bila kuhudumia jamii sidhani kama maisha yatakuwa yana maana, tuihudumie jamii ili kuyapa thamani na maana maisha yetu,” amesema.

7 comments

Comments are closed.