Mashindano ya ubingwa wa taifa ngumi kuanza Juni 24

MASHINDANO ya Wazi ya Ubingwa wa Taifa ya ngumi yanatarajiwa kuanza Juni 24 na kumalizika Juni 29, 2024 katika Chuo Cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam (DPA).

Mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) yanatarajiwa kushirikisha wachezaji huru na wa kutoka klabu mbalimbali za vyombo vya ulinzi na usalama zikiwemo za JWTZ, JKT, Magereza na wenyeji Polisi.

Rais wa BFT Lukelo Willilo, amesema kamati ya ufundi ya Timu ya Taifa ya Ngumi ‘Faru Weusi wa Ngorongoro’ itatumia mashindnao hayo kuboresha kikosi ili kujiandaa na mashindano mbalimbali ya kimataifa yaliyobakia mwaka huu yakiwemo Ubingwa wa Afrika kwa wakubwa na vijana – Conakry Guinea, Ubingwa wa Dunia kwa Wanawake Kazakhstan, Michezo ya Urafiki ya Dunia-Urusi na Mashindano ya Kanda ya tatu ya Afrika.

“Natoa wito kwa wachezaji wajitokeze kwa wingi kushiriki mashindano haya yenye fursa kubwa ya kutambulisha vipaji vyao katika jamii na kwa wale wazoefu kuonyesha umahiri wao Zaidi,”amesema.

Kaimu Katibu na Mwenyekiti wa kamati ya Waamuzi na Majaji Mafuru Mafuru amesema: “Maandalizi yanaendelea vizuri, tunawaomba wadau na wafadhili wajitokeze zaidi kushirikiana na Shirikisho kufanikisha mashindano haya kwa maslahi mapana ya mchezo wa ngumi nchini”

Katika historia ya mchezo wa ngumi, mashindano hayo ndio yameibua nyota wengi wakiwemo Selemani Kidunda, Yusuf Changalawe, Haruna Swanga, Emilian Patrick, Musa Maregesi, Mbonabucha, Kassim Mbundwike, Galiatano, Zulfa Macho na wengine wengi

Habari Zifananazo

Back to top button