Mashirika 31, halmashauri 110 kicheko ripoti ya CAG

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni miongoni mwa taasisi za umma 31 zinazojiendesha kibiashara zilizofanya vizuri katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2023/2024.

Pia Kichere amesema halmashauri 110 pia, zimeng’ara katika ripoti hiyo kwa kuvuka malengo katika ukusanyaji wa mapato.

Kichere alisema Ikulu Dar es Salaam kuwa mashirika ya umma 31 yanayojiendesha kibiashara yalipata faida katika kipindi cha mwaka 2023/2024 na kuipongeza serikali kutokana na juhudi zake za kuwezesha mashirika hayo hadi kutengeneza faida hiyo.

Alitaja baadhi ya mashirika hayo na faida waliyotengeneza kuwa ni TPDC lililopata faida ya Sh bilioni 248.75, NHC (Sh bilioni 242.9) na TPA Sh bilioni 140.48.

Kichere alisema baadhi ya mashirika ya umma yalipata hasara hali inayoonesha kuna changamoto za kiutawala na kiuongozi.

Ameshauri ufanyike ufuatiliaji wa karibu na kuchukuliwa hatua za haraka za kiusimamizi kuhakikisha yanafikia viwango vya tija na ufanisi vinavyotarajiwa.

“Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya Shilingi bilioni 224 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 102 mwaka uliopita. Hasara hii ilichangiwa na kupungua kwa makato ya usafirishaji kutokana na uhaba wa vichwa vya treni na mabehewa pamoja na mvua kubwa iliyosababisha kufungwa kwa njia kwa miezi minne,” alisema Kichere.

Alisema TRC ilipokea ruzuku ya Sh bilioni 29.01 na akasema kama ruzuku hiyo isingetolewa shirika lingepata hasara ya Sh bilioni 253 akisisitiza taarifa hiyo ni ya kipindi cha kabla ya kuanza kutumika kwa treni ya reli ya kisasa (SGR).

Kichere alipendekeza TRC iboreshe utendaji wake ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na ipunguze gharama kwa kutekeleza mpango wa kupata injini na mabehewa.

Alisema Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilipata hasara ya Sh bilioni 91.8 ikilinganishwa na Sh bilioni 56.6 ya mwaka 2022/2023.

Mashirika mengine na hasara zake kwenye mabano ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) (Sh bilioni 27) na Shirika la Posta Tanzania (Sh bilioni 23). Kichere alisema kaguzi 1,485 zilifanyika mwaka 2023/24 ambapo kati ya hizo, 1,301 zinahusu hesabu za fedha, kaguzi 15 zinahusu ufanisi, 52 ni kaguzi maalumu na kiuchunguzi huku 105 zikihusu mifumo ya Tehama na kaguzi 12 ni za kiufundi.

Alisema mwaka 2023/24 ofisi ya CAG ilitoa hati 1,301 ikilinganishwa na hati 1,209 zilizotolewa mwaka 2022/23.

Kati ya hati hizo, 1295 ni hati safi sawa na asilimia 99.5 wakati hati za mashaka ni tano sawa na asilimia 0.4 na hati mbaya ni moja sawa na asilimia 0.1.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button