Mashujaa wetu sasa kurejea Alhamisi asubuhi

DAR ES SALAAM; TIMU ya Taifa ya mpira wa miguu ya (Taifa Stars), ambayo ilikuwa irejee nchini Jumatano Januari 7, 2026, sasa itarejea Alhamisi Januari 8, 2026.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema mabadiliko hayo yana lengo la kuiwezesha timu hiyo kuwasili muda mzuri ambao utatoa nafasi kwa Watanzania kuwapokea na kuwapongeza wachezaji kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya wakiwa katika mashindano AFCON2025 yanayoendelea nchini Morocco.
Msigwa amesema timu itawasili siku hiyo saa 4 asubuhi na itapokelewa na wananchi wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi.
Msigwa ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kuwashangilia na kuwapongeza mashujaa hao kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya nchini Morocco.



