Masuala 10 yatakayopewa msukumo haya hapa

DODOMA; WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameeleza masuala 10 yatakayopewa msukumo kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi, unapunguza umaskini, unazalisha ajira nyingi, unaleta ustawi na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.

Akiwasilisha bungeni leo Juni 13, 2024, Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.Prof Mkumbo amesema:

“Katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi wetu unakuwa jumuishi, unapunguza umaskini, unazalisha ajira nyingi, unaleta ustawi na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi, ninaomba kusisitiza masuala kumi (10) ambayo Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa CCM, itayapa msukumo wa kipekee katika mwaka ujao wa fedha.

“Kuendelea kuwekeza katika kukuza uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu bora, matumizi ya mbolea, kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya zana za kisasa katika kilimo.

“Kuweka na kutekeleza mkakati wa kuchochea uwekezaji katika viwanda vyenye kulenga kuzalisha bidhaa zitakazoifanya nchi ijitosheleze kwa mahitaji ya bidhaa muhimu na kukuza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.

“Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, hususan tukilenga kuweka mazingira maalumu ya kukuza na kuimarisha biashara na uwekezaji mdogo na wa kati (small and medium enterprises),” amesema Waziri Mkumbo.

Ametaja masuala mengine kuwa ni kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya raslimali za taifa, zikiwemo gesi, madini, misitu, bandari, maziwa na kusema kuwa mwelekeo wa kisera wa Serikali ya CCM ni kutumia raslimali hizo kama msingi wa kujenga uchumi wa viwanda kwa kuweka mkazo katika kuongeza thamani mazao yatokanayo na raslimali za asili za Taifa.

“Kwa kuzingatia nafasi ya madini katika kuendelea kukuza ujazo wa mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi, na kwa kuzingatia umuhimu wa madini ya kimkakati (strategic mineral resources-SMR) katika kutimiza azima ya dunia ya kuzalisha nishati safi na salama kwa mazingira, tutaweka mazingira mahususi kwa lengo la kuvutia wawekezaji watakaokuwa tayari kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini, hususan katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha betri za magari na mitambo.

“Kwa kuzingatia kuwa raslimali watu ndio injini ya maendeleo na ndio raslimali kubwa zaidi tuliyo nayo kama Taifa, na kwa kuzingatia idadi kubwa (76%) ya watoto na vijana chini ya umri wa miaka 35 katika nchi yetu, serikali itaendelea kuwekeza katika kuhakikisha kuwa nchi yetu ina raslimali watu wa kutosha na wenye ubora unaokidhi mahitaji ya dunia ya leo na kesho. Hivyo basi, elimu na mafunzo itaendelea kuwa kipaumbele mama katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu.

“Kwa kuzingatia nafasi na umuhimu wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, pamoja na miundombinu ya kidigitali, katika kuchochea maendeleo ya uchumi, Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi na utunzaji wa miundombinu hii kwa kushirikiana na sekta binafsi.

“Kuendelea kuimarisha uzalishaji wa nishati kama nyenzo muhimu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, pamoja na kutekeleza kikamilifu mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za kutosheleza za jamii, zikiwemo afya, maji na umeme, hususan katika maeneo ya vijijini,” amesema.

Amesema kwa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya wananchi wanaishi vijijini (65%), na katika kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi, Serikali itaweka mkazo maalum katika kuchochea maendeleo vijijini kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button