Matamanio, matarajio Dira 2050 hadharani
WANANCHI na wadau mbalimbali nchini wamebainisha matamanio na matarajio yao ya maendeleo kuelekea mwaka 2050 yakiwa ni pamoja na uchumi bora unaostawi, kuboresha maisha yao na huduma bora za kijamii hususan elimu na afya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo amebainisha yao katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050 na hatua zinazofuata.
Matarajio na matamanio mengine ya wananchi yaliyobainika wakati wa mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili
ya kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni utawala bora, utoaji haki, ulinzi na usalama, maendeleo ya
teknolojia na ubunifu, ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.
Profesa Kitila amesema katika maoni hayo, wananchi wamebainisha vipaumbele mbalimbali ambavyo ni pamoja na kilimo, uzalishaji viwandani, ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
“Wananchi na wadau walitaja sekta tano za kuzingatiwa kama vipaumbele vya kitaifa kuelekea mwaka 2050 ambavyo ni kilimo, uzalishaji viwandani (kuongeza thamani), miundombinu, huduma bora za jamii, madini, mafuta na gesi,” amesema Profesa Kitila.
Amesema katika ukusanyaji wa maoni hadi kufikia Oktoba mwaka huu, wananchi na wadau 1,170,970 walitoa maoni yao kwa njia mbalimbali, zikiwemo tafiti katika ngazi ya kaya na kuwafikia watu 15,483, ujumbe kwa njia ya simu (USSD) watu 1,118,978 na tovuti watu 13,459.
“Asilimia 81 ya waliotoa maoni kwa njia ya simu walikuwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 na inafurahisha kwa sababu miaka 25 ijayo hawa vijana ndio watakuwa kwenye nafasi tulizonazo, ndio watakuwa
wanaongoza nchi,” ameeleza.
Njia zingine ni makongamano 12 yaliyohudhuriwa na watu 22,779, mahojiano mahususi na ya kina na viongozi mbalimbali waliopo madarakani na waliostaafu ambako walifikiwa viongozi 44, mikutano na semina watu 220 pamoja na nyaraka 33 zilizokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali.
Profesa Kitila ameeleza kuwa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Desemba 11, mwaka huu mjini Unguja.
“Uzinduzi huo utaenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wananchi na wadau. Awamu hii itahusu maoni ya uhakiki wa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendelep 2050,” amesema
Profesa Kitila.
Ameongeza kuwa baada ya kukusanya maoni ya uhakiki, Januari 18, 2025 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atazindua
rasimu ya pili ya dira ambayo itakuwa imejumuisha maoni ya wadau mbalimbali katika hatua ya uhakiki na kuhitimisha mchakato wa wananchi.
Amesema baada ya hapo, utaingia mchakato wa kiserikali na kibunge ambapo taarifa na rasimu ya dira itajadiliwa na kufanyiwa uamuzi katika vyombo vya uamuzi vya serikali (makatibu wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango na
Baraza la Mawaziri).
“Kati ya Aprili/Mei 2025, Rasimu ya Dira 2050 itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishiwa rasmi kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Bunge kisha Rais atazindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Mei/ Juni 2025 kabla Bunge la 12 halijavunjwa rasmi Juni 30, 2025,” amefafanua Profesa Kitila.



