Matampi Mchezaji Bora Ligi Kuu Februari

DAR ES SALAAM: MLINDA lango wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemkrosia ya Congo (DRC) na klabu ya Coastal Union ya Tanga, Ley Matampi amechaguliwa Mchezaji Bora wa mwezi Februari katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Matampi ametwaa tuzo hiyo baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa kucheza dakika 270 za michezo mitatu bila kuruhusu bao.
Rekodi zinaonesha, mwezi Februari, Coastal ilitoka suluhu ya 0-0 ugenini dhidi ya klabu ya KMC iliyo chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Coastal, ikashinda nyumbani Mkwakwani Tanga, bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, halkadhalika ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kipa huyo amewashinda kiungo Mudathir Yahya Abbas wa Young Africans na mshambuliaji Samson Mbangula wa Prisons alioingia nao fainali huku akiwa ameisaidia Coastal kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya nne katika msimamo wa ligi.