Mavunde amaliza mgogoro wa wachimbaji wadogo Chamwino
DODOMA: WAZIRI Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amemaliza mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini uliodumu kwa mwaka mmoja katika Kitongoji cha Mafurungu ,Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza katika Mkutano na wachimbaji wadogo hao, Mavunde amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika ukuaji wa uchumi wa taifa hivyo inafanya kila juhudi kuhakikisha wachimbaji wadogo wapo katika mazingira salama.
Amesema, mazingira bora ya uchimbaji ni pamoja usalama katika uchimbaji, kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa lakini pia kuwa na taarifa sahihi za uwepo wa madini ili kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.
Amesema, kutokana na umuhimu katika sekta ya madini, wamefunga rasmi mgogoro kwa kuwapatia leseni nne za uchimbaji ili kila mmoja achimbe bila kuwepo na mgogoro wowote katika kitongoji cha Mafurungu.
Aidha, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji katika maeneo yao ya kazi ambapo katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya kitongoji cha Mafurungu tayari ametoa ahadi ya mifuko 200 ya Saruji na kuwa Balozi wa kujitolea kwa eneo hilo.
Naye, Kamishna wa Madini Dk. AbdulRahm Mwanga ameupongeza uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa madini kupitia Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mafurungu (UWAWAMA) kwa kukubali na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mavunde na kuweza kufuta sintofahamu zote zilizokuwepo awali.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Mtera Livingstone Lusinde ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya madini kwa utatuzi wa mgogoro huo na kuwataka wachimbaji hao kuongeza uzalishaji zaidi ili kuinua mapato ya halmashauri na serikali Kuu.
Awali , Meneja Mgodi Mbwana Mosses akisoma taarifa ya mafanikio ya Chama cha UWAWAMA kuhusu uzalishaji wa dhahabu amesema kuwa hadi sasa chama kupitia migodi yake kimeweza kuzalisha kiasi cha gramu 11093.19 za dhahabu ambazo zina thamani ya Sh bilioni 1.331 na kulipa Mrabaha wa Sh milioni 79.888.