Mavunde aongoza mkutano chama cha migodi

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameongoza mkutano maalum baina ya Serikali na Chama cha Migodi Tanzania, ambapo wadau wote wa sekta ya madini wamekutana kujiandaa kwa maonesho yatakayofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini.
Madhumuni ya mkutano huo ni kuiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa na kuvuta uwekezaji, hususan katika maeneo ya utafiti, na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika huduma na usambazaji wa bidhaa mbalimbali.
Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa sauti moja kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuitangaza nchi nakuonyesha matumaini kuwa fursa hii italeta uwekezaji mkubwa, kuongeza ajira kwa Watanzania, na kuchangia katika kuongeza mapato ya taifa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali na sekta binafsi kukaa chini pamoja kwenye mkutano wa namna hii, na inaashiria hatua muhimu kuelekea ushirikiano wenye tija.
Mwenyekiti wa Chama cha Migodi, Philbert Rweyemamu, ametoa wito kwa Watanzania wote wanaoshiriki maonesho hayo kuhakikisha wanafanya bidii katika kutafuta wawekezaji. Amesema lengo ni kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuongeza uwekezaji na kuitangaza nchi.
Ushirikiano huu unalenga kuwawezesha wote kufaidika na rasilimali za madini zilizobarikiwa nchini Tanzania.