Mavunde aonya maofisa madini wa mikoa

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua kali maofi sa madini wakazi wa mikoa, ambao ofi si zao zitabainika kuhusika au kusababisha migogoro katika shughuli za uchimbaji wa madini.
Amesisitiza ulazima wa kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za madini katika utekelezaji wa majukumu yao. Mavunde ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi kikao cha menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha wakurugenzi, mameneja na maofisa madini wakazi wa mikoa.
Kikao hicho kimelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya madini. Mavunde alisema kumekuwapo na baadhi ya maofisa katika ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.
“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo,” alieleza Mavunde. SOMA: Mavunde: Leseni za madini kwa vikundi, si mtu mmoja
Ameagiza maofisa hao kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji. Katika hatua nyingine, amewataka maofisa hao kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi ili hatua za kisheria zichukuliwe, ikiwamo kuandikiwa hati za makosa na kufutiwa leseni hizo.
Aidha, amemtaka mkurugenzi wa leseni kuwasilisha orodha ya kampuni zenye leseni kubwa za utafiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake. “Mimi kwa kushirikiana na naibu waziri tutahakikisha tunafuatilia kila leseni. Zile zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa na maeneo hayo kupewa wachimbaji wadogo wa madini,” alisema Mavunde.
Kadhalika, amemtaka katibu mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, mwaka huu mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Vilevile,amewataka wamiliki wa leseni za madini kuzifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua, ikiwamo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati. Pia, amewaagiza maofisa madini wakazi wa mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, mwaka huu taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Programu ya Uchimbaji kwa Kesho Bora (MBT).
Katika kuimarisha utendaji kazi, Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwao, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao.
Pia, Mavunde ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli kwa miaka sita mfululizo, akieleza kuwa makusanyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh trilioni 1.071 mwaka 2024/2025, mafanikio yanayotokana na maboresho ya sheria, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, mwaka huu serikali tayari imekusanya Sh bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la Sh trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026. “Hii ni hatua nzuri na nina imani kubwa kuwa tutavuka lengo lililowekwa na serikali kabla ya Juni 30, 2026,” alibainisha.
Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amempongeza Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili sekta ya madini izidi kuimarika.



