Twiga Minerals Yaipa Tanzania Nuru Mpya ya Maendeleo

TANZANIA inaendelea kung’ara kimataifa kupitia sekta ya madini, huku Twiga Minerals Corporation yenye ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Barrick ikichukua nafasi ya kipekee katika kukuza uchumi wa taifa.

Kupanda kwa uzalishaji wa dhahabu katika migodi ya North Mara na Bulyanhulu, kunakokwenda sambamba na ongezeko la bei ya dhahabu duniani, kumeifanya Twiga Minerals kuwa injini muhimu ya mapato, ajira na maendeleo ya kijamii mwaka 2025.

Uwekezaji na ufanisi wa kampuni hiyo umeleta mageuzi yanayoonekana katika ukuaji wa miji, kuboreshwa kwa huduma za kijamii na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika jamii zinazozunguka migodi hiyo.Kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu katika migodi ya North Mara na Bulyanhulu kunakoendeshwa chini ya ubia huu kumeleta matokeo chanya kwa uchumi wa taifa.

Katika robo ya tatu ya mwaka 2025, migodi hiyo iliongoza kwa ukuaji wa uzalishaji kwa asilimia nane ikilinganishwa na robo iliyotangulia, ikiendelea kuthibitisha umuhimu wa Twiga Minerals katika sekta ya madini nchini. Barrick Gold Corporation, kupitia migodi hiyo miwili, imeendelea kuwa chanzo kikuu cha mchango kwa pato la taifa kupitia kodi, ajira, usafirishaji na malipo kwa watoa huduma za ndani.

Kampuni hiyo imeingiza zaidi ya dola bilioni 4.79sawa na zaidi ya shilingi trilioni 12 katika uchumi wa Tanzania, hatua iliyowezesha rekodi mpya katika malipo na usafirishaji. Miji kama Kahama na Tarime pamoja na vijiji vya Nyamongo na Kakola imebadilika kwa kiasi kikubwa kiuchumi, huku mzunguko wa fedha kutokana na shughuli za migodi ukichochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na kuibuka kwa wajasiriamali wapya.

Fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zimechangia ujenzi wa miundombinu bora hasa kwenye elimu, afya, maji na barabara, na kuimarisha ustawi wa wakazi katika maeneo ya karibu. SOMA: Katavi yafungua fursa mpya uwekezaji madini

Katika robo ya pili ya mwaka 2025 pekee, takribani dola milioni 558 (zaidi ya shilingi trilioni 1.4) ziliingizwa kwenye uchumi kupitia ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani. Kwa mujibu wa Barrick, asilimia 90 ya ununuzi wote hufanywa na kampuni za Kitanzania, nyingi zikiwa ni za wazawa, jambo linaloendelea kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira.

Kampuni hiyo pia imeajiri Watanzania kwa asilimia 96 ya jumla ya wafanyakazi 6,185, ambapo asilimia 53 wanatoka vijiji vinavyozunguka migodi ya North Mara na Bulyanhulu. Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk. Melchiory Ngido, anabainisha kuwa asilimia 100 ya nafasi za juu za uongozi katika migodi hiyo zinashikiliwa na Watanzania, huku uwakilishi wa wanawake ukiwa asilimia 13.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button