DAR ES SALAAM; Mawasiliano ya Barabara kuu ya Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara yamerejea eneo la Somangafungu mkoani Lindi, baada ya daraja la Somanga linalounganisha barabara hiyo kukatika na kusababisha barabara hiyo kufungwa kwa saa kadhaa.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Nzengo, amesema tayari magari ya abiria na mizigo na vyombo vingine vya usafiri vimeruhusiwa na kuanza kupita upande mmoja katika daraja hilo, ambalo lilikuwa halipitiki tangu usiku wa kuamkia leo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
“Tumekamilisha kazi awamu ya kwanza, wananchi na magari wameruhusiwa kuanza kupita.
Tunawashukuru wananchi kwa uvumilivu na tunaomba waendelee kuiamini serikali ipo kazini kwa ajlili yao,” amesema Mhandisi Nzengo.
Mapema Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alieleza kuwa jitihada kubwa zinaendelea za kurudisha mawasiliano ya barabara eneo la Somangafungu na kuagiza timu ya wataalam kutoka TANROADS kuhakikisha hadi kufikia mchana Machi 25, 2024 mawasiliano yawe yamerejeshwa na magari yaanze kupita katika daraja hilo.